Imeeleza kuwa pamoja na ongezeko la uzalishaji wa kuku, ulaji wa nyama kwa mtu mmoja kwa mwaka bado ni mdogo kitaifa ambapo takwimu zinaonesha ni kilo 15 kati ya 50 zinazopendekezwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Aidha, imeelezwa kiwango cha sasa cha ulaji wa mayai kwa mtu mmoja kwa mwaka ni 106 wakati mapendekezo ya FAO kiasi kinachotakiwa ni 300.
Hayo yalibainishwa juzi jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati wa kikao cha Wizara na wadau wa tasnia ya kuku na alisema juhudi zinahitajika kuendelea kuhamasisha wananchi kutumia nyama ya kuku ili kufikia kiwango kinachoshauriwa na FAO.
Ulega alisema takwimu za mwaka 2021/2022, Tanzania ina kuku milioni 92.8 ambapo kuku wa asili ni milioni 42.7 na kuku wa kisasa ni milioni 50.1.
Alisema kaya zinazojishughulisha na kilimo na ufugaji ni zaidi ya kaya milioni 7, kati ya hizo kaya zaidi ya milioni 4 sawa na 55.3 wanafuga kuku, hii inaonesha ufugaji wa kuku ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wengi nchini.
“Ulaji wa nyama kwa sasa ni kilo 15 kwa mtu kwa mwaka, aidha kati ya hizo ni kilo 2 tu zinatokana na nyama ya kuku,hali kadhalika ulaji wa mayai kwa sasa ni 106 kwa mtu kwa mwaka takwimu ambazo zipo chini,”alisema Ulega.
Alisema sekta ya kuku imekua kwa kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na kuwepo kwa soko linalotokana na ongezeko la watu na kipato, uwekezaji na uwepo wa mazingira bora katika tasnia ya hiyo.
Ulega alitaja sababu nyingine ni kuwepo urahisi wa kufuga kuku na uwezekano mkubwa wa kuwamiliki kuliko wanyama wakubwa, uwepo wa Taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo kwa vijana na akina mama na vikundi mbalimbali ambao wengi wamejizatiti katika biashara ya kuku.
Alisema kuwepo kwa faida zote hizo na soko kubwa la kuku hapa nchini, suala la upatikanaji wa vifaranga na vyakula vya kuku limekuwa likipanda na kushuka katika msimu wa mwaka.
“Katika kipindi cha mwaka 2019 ulipozuka ugonjwa wa Corona ilileta athari kubwa katika mnyororo wa thamani wa tasnia ya kuku. Pamoja na changamoto hizi nina imani katika kikao hiki tutajadili kwa mapana yake namna ambavyo sekta mbalimbali zitashiriki kwenye utatuzi wa changamoto zilizopo katika tasnia hii,”alisema.
Ulega alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo kwa michango yao katika Sekta ya mifugo.
Aidha, alitoa rai kwa taasisi za kifedha kuona namna ya kuwekeza katika mnyororo wa thamani ili kuchagiza ya ustawi wa tasnia ya kuku, kupitia ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi (PPP).