Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kuacha matumizi holela holela ya Dawa ili kuepuka usugu wa vimelea dhidi ya dawa hususani za antibaotik kushindwa kufanya kazi ipasavyo na kugharimu maisha na nguvu kazi ya Taifa.
Waziri amesema hayo Juni 19, 2024 Jijini Arusha wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Afya ya nchi zacMashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) ambapo mgeni Rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango.
“Usugu wa vimelea vya magonjwa Dhidi ya Dawa ni janga kubwa ambalo jamii ya Watanzania inapaswa kupambana nalo kwa dhati kwa kuwa madhara yake ni Mkubwa na yanagharimu fedha nyingi.”
“ikiwa umeandikiwa dawa unywe kwa siku Tano basi maliza siku zote Tano, zingatia matumizi sahihi ya dawa hususani za antibaiotik na usitumie dawa bila ya kuandikiwa na daktari au mtaalam wa mifugo, unakuta dawa za mifugo anapewa binaadamu tuepuke kutengeneza janga kubwa ambalo litakwenda kugharimu Sekta ya Afya kwa siku za usoni kwa kuendelea na matumizi holela ya dawa.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy ameongeza kuwa madhara ya matumizi holela ya dawa hupelekea mgonjwa kukaa hospitalini ama kuugua kwa muda mrefu bila kupona lakini pia mgonjwa kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kujiuguza na hata kupoteza maisha kutokana na changamoto hiyo ya usugu wa vimelea dhidi ya Dawa
Kuongezeka kwa mzigo wa magonjwa Yasiyoambukiza katika ukanda huu, Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) imejipanga kuja na Tafiti zitakazo saidia kuja na ushahidi wa kisayansi utakao saidia mbinu sahihi za kupambana na magonjwa hayo na kuweka sera nzuri zitakazosaidia kufikia suala la Afya kwa wote.
Aidha, amesema katika miaka 50 ya Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) kuna mengi makubwa ya kujivunia kwa kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi katika masuala ya afya na nchi za ukanda wa mashariki, kati na kusini mwa Afrika wataendelea kuongeza mashrikiano baina ya nchi wanachama ili kubuni na kuendeleza afua zaidi za Afya ambazo zitasaidia kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta hiyo barani Afrika
Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) wametusaidia sana sisi kama Tanzania katika kufanya tafiti za kisayansi kuhusu magonjwa ya kuambukiza lakini kubwa ni kuweza kutusaidia tukatengeneza mpango mkakati wa kupambana na magonjwa sugu pamoja na majanga kwa kujitathimini katika kupambana na magonjwa makubwa ya kuambukiza kama Ebola, Covid na homa ya bonde la ufa na kudhamini masomo kwa wataalamu wa Afya.” Amesema Waziri Ummy