Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Ummy:Maambukizi mengine ya TB yanapatikana kwenye mabweni - Mwanzo TV

Ummy:Maambukizi mengine ya TB yanapatikana kwenye mabweni

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu, amewataka wakuu wa wilaya nchini humo kushirikiana na waganga wakuu wa wilaya kuweka utaratibu wa kuzitembelea shule za bweni ili kubaini mlundikano wa wanafunzi katika mabweni hayo na kuchukua hatua ili kudhibiti maambukizi ya kifua kikuu.

Waziri Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo Machi 24, 2022 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu (TB) duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Tanga.

Amesema kumekuwa na mlundikano mkubwa wa wanafunzi katika shule za bweni ambao unaweza kusababisha athari za kiafya kwa wanafunzi.

“Wekeni utaratibu wa kutembelea Kwenye shule za bweni na kuchukua hatua kwani maambukizi mengine yanapatikana huko mashuleni,” amesema.

Pamoja na mambo mengine ametoa katazo kwa hospitali zote nchini humo kuacha tabia ya kutoza fedha kwa wanafunzi wanaokwenda kupima afya kwa ajili ya kujiunga na shule au vyuo kwani kwa kufanya hivyo wanakiuka utaratibu.

“Ni kosa kuchukua fedha kwa ajili ya ujazaji fomu ya uchunguzi wa afya kwa wanafunzi huduma hii ni bure hivyo wapimwe bure, siyo mnasaini bila kuwafanyia uchunguzi wa afya kama fomu inavyoelekeza kwa kufanya hivyo mnasababisha watoto kuambukizana maradhi,” amesema Waziri Ummy.

Aidha, amesema serikali imeandaa mpango wa kuwawezesha kiuchumi kaya masikini zinazohudumia wagonjwa wa kifua kukuu kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 .

Ummy amesema lengo la serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kuutokemeza ugonjwa huo ambao mpaka sasa wagonjwa 47,000 bado hawajafikiwa.

Aidha Waziri Ummy ametoa agizo pia kwa waganga wakuu wote nchini kuwabaini wenye maduka makubwa ya dawa ambao wanauzia wananchi dawa kali bila cheti kutoka kwa mtabibu.

“Salamu ziwafikie wenye maduka makubwa ya dawa ninayo majina ya maduka makubwa mawili nimepata taarifa wanauza dawa kiholela kwa kutoa dawa kali ambazo hazitakiwi kutolewa bila cheti cha daktari nasema nitawachukulia hatua kali hili halikubaliki,” amesema.