Ummy:Punguzeni semina wananchi wapate huduma

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amewataka wataalamu wa afya nchini humo kupunguza semina ili kuwa na muda zaidi wa kutoa huduma bora za matibabu kwa wananchi.

Waziri Ummy ameyasema  hayo katika ziara yake mkoani Simiyu wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Dkt. Yahaya Nawanda.

“Wataalamu wa afya punguzeni semina maana mmekuwa na semina nyingi hadi kupelekea wagonjwa kukosa huduma kwa wakati na kumekuwa na msomgamano mkubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya sababu ya semina”, amesema.

Aidha, amesema kuwa kwa mara ya kwanza Serikali imetoa hela za dawa kwa asilimia 100 kwa mkoa wa Simiyu, hivyo amevitaka vituo vyote vya Afya kuwa na dawa zote muhimu ili kumsaidia mwananchi kupata huduma za matibabu kwa wakati ambapo kwa mwaka 2022/2023 mkoa huo umepata bajeti ya bidhaa za afya shilingi Bilioni 3.4 na shilingi Bilioni 8.1 kwa ajili ya vifaa tiba pekee.

“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kila kitu katika sekta ya Afya ikiwemo majengo, vifaa tiba, kuajiri wataalamu na sasa ni jukumu letu wataalamu kutoa huduma bora kwa wananchi kwani ndio dhamira ya Serikali,” amesema.

Pia, Waziri Ummy ametoa rai kwa watoa huduma nchini kuzingatia utumiaji wa lugha nzuri, weledi na maadili na kuzingatia viapo vya wataalamu wa afya wakati wa kuwahudumia wananchi.