Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu uvamizi ardhi na makazi ya jamii ya Wamaasai unaoendelea na unaoambatana na ukosefu wa uwazi katika kushauriana na jamii hiyo wakati wa kufanya maamuzi.
Mwenendo huu, hivi karibuni ulisababisha vurugu za vyombo vya usalama dhidi ya Wamaasai waliokuwa wakilinda ardhi ya mababu zao katika Tarafa ya Loliondo Wilaya ya Ngorongoro, kaskazini mwa Tanzania.
“Tunasikitishwa sana na taarifa za matumizi ya risasi za moto na mabomu ya machozi yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya Tanzania tarehe 10 Juni 2022, na kusababisha takriban watu 30 kupata majeraha madogo hadi mabaya kutokana na risasi za moto na kifo cha afisa wa polisi,” walisema wataalamu hao. .
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana tarehe 6 Juni, kufuatia kikao cha faragha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha alitangaza uamuzi wa kugeuza eneo la kilomita za mraba 1,500 na kilomita za mraba 4,000 za ardhi ya kijiji inayojumuisha Pori Tengefu la Loliondo kuwa pori la akiba.
Mabadiliko hayo yangemaanisha kufukuzwa kutoka kwenye vijiji vya Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo, na Arash, ambavyo vinaweza kuhamisha wenyeji wa Kimasai takribani 70,000.
Uamuzi huo umekuja licha ya zuio la mwaka 2018 la Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kwamba tarehe 22 Juni Mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la kisheria la kuwaondoa Wamasai katika ardhi yao katika eneo hili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba mnamo tarehe 7 na 8 Juni, karibu wanachama 700 wa vikosi vya usalama waliwekwa katika maeneo matano katika eneo hilo, ambapo waliweka kambi za mahema kuanza kuweka mipaka ya kilomita za mraba 1,500.
Na tarehe 9 Juni polisi waliweka alama za kubainisha eneo la hifadhi, lakini Wamasai wa eneo hilo waliziondoa na kukaa usiku kucha kulinda eneo hilo.
Vikosi vya usalama viliporejea alfajiri, walianza kufyatua risasi za moto na kuwarushia Wamasai vitoa machozi.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa hali nyingine imekuwa ikijitokeza katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, ambako mamlaka imeripotiwa kuendeleza mipango ya kuwaondoa Wamasai wanaokadiriwa kufikia 80,000 kutoka katika ardhi ya mababu zao.
Wawakilishi wa Wamaasai walisema kuwa hakukuwa na juhudi za kweli za kushauriana nao na kwamba wanaona nia na mpango wa kufukuzwa kutokana na taarifa za chini chini zinavyoeleza.
Ni tarehe 9 Februari tu Bunge lilifanya kikao maalum kujadili haki ya Wamasai kuishi katika eneo hilo, ambayo imehakikishwa kisheria tangu miaka ya 1950.
Serikali ilisema hakuna mpango wa kuwaondoa Wamasai kwa nguvu lakini kumekuwa na taarifa za kuongezeka kwa polisi na unyanyasaji katika vijiji vya Wamasai, na kuwashauri wenyeji “kujitolea” kuhamishwa kwa sababu hawatakuwa na chaguo ila kuhama.
“Katika hali kama hiyo, inaonekana haiwezekani kuhakikisha kwamba kuhamishwa kwa Wamasai kutoka eneo hilo hakutakuwa sawa na kufukuzwa kwa lazima na kuhama kiholela chini ya sheria za kimataifa,” walibainisha wataalam wa Umoja wa Mataifa.
“Tuna wasiwasi na mipango ya Tanzania ya kuwahamisha takriban Wamasai 150,000 kutoka Hifadhi ya Ngorongoro na Loliondo bila ridhaa yao kama inavyotakiwa chini ya sheria na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu. Hii itasababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa, na inaweza kuwa kunyang’anywa mali, kufukuzwa kwa lazima na uhamishaji holela uliopigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa, ” Walionya wataalam wa Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa
“Inaweza kuhatarisha maisha ya Wamasai kimwili na kiutamaduni kwa jina la ‘uhifadhi wa asili’, utalii wa safari na shughuli za uwindaji pamoja na kupuuza uhusiano ambao Wamasai wamekuwa nao”
“Tunaiomba Serikali ya Tanzania kusitisha mara moja mipango ya kuwahamisha wananchi wanaoishi Loliondo na Hifadhi ya Ngorongoro na kuanza mashauriano na Wamasai ikiwa ni pamoja na kuwasiliana moja kwa moja na Baraza la Wafugaji la Ngorongoro ili kuainisha kwa pamoja changamoto zilizopo katika uhifadhi wa mazingira. na njia bora za kuzitatua, huku tukidumisha mkataba unaozingatia haki za binadamu katika uhifadhi,” walisema wataalamu hao.
Pia walizitaka mamlaka za Tanzania kuonyesha uwazi kwa kukubali maombi ya uchunguzi kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kujibu maombi ya ziara ya nchi kutoka kwa Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Makazi ya Kutosha na Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili.
Mnamo 2010, Hifadhi ya Ngorongoro ilitambuliwa na UNESCO kama Tovuti ya Urithi wa Dunia kwa thamani yake ya kitamaduni. Wakikumbuka kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yana wajibu wa kusimamia haki za binadamu katika kazi zao, wataalamu hao wameiomba Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO (WHC) kusisitiza tena kwa Serikali ya Tanzania kuwa mipango inayohusu eneo la Hifadhi ya Ngorongoro inazingatia viwango husika vya haki za binadamu.
Wataalamu hao walikumbuka kuwa Julai 2021 WHC ilipendekeza Tanzania ialike Ujumbe wa Ushauri wa WHC ili kutafakari mipango yake ya eneo hilo.
Wataalam hao hapo awali walitoa dukuduku lao kuhusu suala hili kwa Serikali ya Tanzania, Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO, Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira, na Baraza la Kimataifa la Makumbusho.