Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyozinduliwa jana kuhusu hatua zilizopigwa katika ufikiaji wa lengo namba 7 la maendeleo endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030 lihusulo nishati , inasema pengo la nishati duniani bado linaendelea kwani watu milioni 675 hawana umeme , huku watu bilioni 2.3 wanategemea nishati hatari za kupikia kwa afya zao na mazingira.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa kwa pamoja na shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, shirika la nishati mbadala IRENA, Idara ya takwimu ya Umoja wa Mataifa UNSD na Benki ya Dunia inasema “Janga la Virusi vya Corona ni chachu kubwa ya kudorora kwa mchakato wa kuelekea ufikiaji wa nishati kwa wote huku ikionya kwamba katika kiwango cha sasa watu milioni 670 watasalia bila nishati ya umeme ifikapo mwaka 2030 wakiwa ni watu milioni 10 zaidi ya ilivyotabiriwa mwaka jana.”
Ripoti hiyo ya toleo la mwaka 2022 “Ufuatiliaji wa SDG 7: Ripoti ya Maendeleo ya Nishati” inaonyesha kuwa athari za janga hili, ikiwa ni pamoja na mashariti ya kufungwa kila kitu, kuathirika kwa minyororo ya usambazaji wa kimataifa, na upotoshaji wa rasilimali za kifedha ili kuweka bei za chakula na mafuta kuwa nafuu, vimeathiri kasi ya maendeleo kuelekea lengo la Maendeleo Endelevu SDG 7 la kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu, ya kutegemewa, endelevu na ya kisasa ifikapo mwaka 2030.
Mchakato unademadema hasa katika nchi zilizo hatarini zaidi na zile ambazo tayari ziko nyuma katika upatikanaji wa nishati.
“Takriban watu milioni 90 barani Asia na Afrika ambao hapo awali walipata umeme, hawawezi tena kumudu kulipia mahitaji yao ya msingi ya nishati.” Imesema ripoti hiyo na kuongeza kuwa athari hizo zimechochewa Zaidi na uvamizi wa urusi nchini Ukraine katika miezi michache iliyopita ambao umesababisha hali ya sintofahamu katika soko la kimataifa la suala la mafuta na gesi na hivyo kupandisha juu gharama za nishati.
Afrika inaendelea kuburuta mkia katika nishati
Afŕika inasalia kuwa bara lenye kiwango kidogo Zaidi cha umeme duniani ikiwa na watu milioni 568 wanaoishi bila umeme.
Kwa mujibu wa ripoti Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ya idadi ya watu walio bila fursa ya umeme ilipanda hadi asilimia 77 mwaka 2020 kutoka asilimia 71 mwaka 2018 ambapo kanda nyingine pia zilishuhudia kupungua kwa sehemu yao ya upatikanaji wa umeme.
Wakati watu milioni 70 duniani kote walipata nishati safi ya kupikia na teknolojia, maendeleo haya hayakutosha kuendana na ongezeko la idadi ya watu, hasa katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ripoti hiyo imebaini kuwa licha ya usumbufu unaoendelea katika shughuli za kiuchumi na minyororo ya usambazaji, nishati mbadala ilikuwa chanzo pekee cha nishati kukua kupitia janga la COVID-19.
Hata hivyo, ripoti inasema mienendo hii chanya ya kimataifa na kikanda katika nishati mbadala imeziacha nyuma nchi nyingi zinazohitaji umeme.
Hili lilichochewa na kupungua kwa mtiririko wa fedha wa kimataifa kwa mwaka wa pili mfululizo, na kushuka hadi dola bilioni 10.9 mwaka 2019.
Ripoti hiyo pia “imegundua kuwa kuongezeka kwa madeni na kupanda kwa bei ya nishati kunazidisha mtazamo mbaya wa kufikia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na umeme kwa wote.”
Makadirio ya sasa yanaashiria kuwa “watu bilioni 1.9 watakosa nishati safi ya kupikia na watu milioni 660 watakuwa bila huduma ya umeme ifikapo 2030 ikiwa hatutachukua hatua zaidi na kuendelea na juhudi za sasa.”
Kauli za mashirika
Fatih Birol, mkurugenzi mtendaji, wa shirika la kimataifa la nishati amesema “Mshtuko uliosababishwa na COVID-19 ulirudisha nyuma maendeleo ya hivi karibuni kuelekea upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia, na kupunguza uboreshaji muhimu katika ufanisi wa nishati hata kama nishati jadidifu zilionyesha mnepo wa kutia moyo. Leo, uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umesababisha mzozo wa nishati duniani, na kuchochea ongezeko kubwa la bei ambalo linasababisha athari mbaya sana katika nchi zinazoendelea kiuchumi. Nyingi ya nchi hizo tayari zilikuwa katika hali mbaya ya kifedha kutokana na mzozo wa COVID-19, na ili kuondokana na matatizo haya na kuweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu kutahitajika ufumbuzi mkubwa na wa ubunifu wa kifedha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.”
Kwa upande wake Francesco La Camera, mkurugenzi mkuu, wa shirika la kimataifa la nishati mbadala au jadidifu anasema “Ufadhili wa kimataifa wa umma kwa nishati mbadala unahitaji ili kuharakisha mchakato hasa katika nchi masikini zaidi, zilizo hatarini zaidi. Tumeshindwa kusaidia wale wanaohitaji sana nishati. Huku ikiwa imesalia miaka minane tu kufikia ukomo wa utimizaji lengo la upatikanaji wa nishati kwa gharama nafuu na endelevu, tunahitaji hatua kali ili kuharakisha ongezeko la mtiririko wa fedha za umma wa kimataifa na kuzisambaza kwa njia ya usawa zaidi, ili watu milioni 733 ambao wameachwa nyuma kwa sasa wanaweze kufurahia manufa ya upatikanaji wa nishati safi.”
Kuna hatua zilimepigwa
Stefan Schweinfest, kutoka idara ya takwimu ya Umoja wa Mataifa akizungumzia mafanikio amesema “Ripoti hiyo ya 2022 imegundua kuwa kuna hatua zilizopigwa kuelekea kufikia nishati ya gharama nafuu, ya kutegemewa, endelevu na ya kisasa kwa wote, ingawa haziko katika kasi ya kutimiza lengo 2030. Mbaya zaidi, miaka miwili ya janga la COVID-19 imeathiri vibaya mtiririko wa uwekezaji wa kimataifa wa kukuza nishati mbadala katika nchi zinazoendelea. Hizi ndizo nchi ambazo zinahitaji uwekezaji zaidi kufikia Lengo la 7, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa takwimu ili kusaidia kufuatilia na kutathmini sera na mikakati ya nishati endelevu.
Benki ya dunia kupitia kwa makamu wake wa Rais wa miundombinu Riccardo Puliti imesema bado ina matumaini “Tunaamini SDG 7 bado ni lengo linaloweza kufikiwa na tunazihimiza serikali na jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za kujumuisha upatikanaji wa nishati kwa wote katika mipango ya mpito ya nishati ya kitaifa, na kuzingatia watu walio mbali zaidi, walio katika mazingira magumu na maskini zaidi wasio na huduma ili kuhakikisha hakuna hata mmoja anayeachwa nyuma.”
Naye mkurugenzi wa idara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na afya wa WHO Dkt.Maria Nerira amesema “Mamilioni ya watu wanauawa kwa magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na homa ya mapafu au nimonia kwa vile bado wanategemea nishati chafu za kupikia na teknolojia ambazo ni vyanzo vikuu vya uchafuzi wa hewa. Wanawake na watoto wako hatarini zaidi kwani hutumia wakati mwingi ndani na nje ya nyumba na kwa hivyo hubeba mzigo mzito zaidi kwa afya na ustawi wao. Kuhamia kwenye nishati safi na endelevu haitachangia tu kuwafanya watu kuwa na afya bora, pia italinda sayari yetu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.”