UNICEF:Ubaguzi wa rangi na ubaguzi dhidi ya watoto umeenea duniani kote.

Taarifa iliyotolewa leo na UNICEF kutoka New York Marekani imeeleza kuwa katika utafiti uliofanywa kwenye nchi 22 za kipato cha chini na cha kati umeonesha jinsi watoto wanavyobaguliwa katika afya, kupata rasilimali zinazotolewa na serikali, na elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema ubaguzi wa rangi na kimfumo unawaweka watoto katika hatari ya kunyimwa haki na kutengwa vitendo ambavyo vinaweza kuwa na athari katika Maisha yao yote.

Bi. Russell amesema “Hii inatuumiza sisi sote. Kulinda haki za kila mtoto hata awe nani, popote anapotoka ndiyo njia ya uhakika ya kujenga ulimwengu wenye amani zaidi, ustawi na haki kwa kila mtu.”

Ripoti hiyo ya utafiti iliyopewa jina la Haki zilizonyimwa: Athari za ubaguzi kwa watoto imeonesha kuwa wale walio katika kundi la kunufaika wameonekana kuwa na uwezekano maradufu wa kuwa na stadi za kimsingi za kusoma. Kwa wastani, wanafunzi walio na umri wa miaka 7 mpaka 14 kutoka kundi lililonufaika zaidi wana uwezekano wa kuwa na ujuzi wa kusoma wa kimsingi zaidi ya mara mbili, kuliko wale wa kundi lisilo na faida zaidi.

Ubaguzi na kutengwa kunazidisha umaskini wa vizazi na vizazi na kusababisha watu kuwa na afya duni, lishe isiyo bora, ujauzito katika umri mdogo, mimba nyingi miongoni mwa wasichana barubaru, uwezekano mkubwa wa kufungwa, na viwango vya chini vya ajira na mapato wakiwa watu wazima.

Kwa mfano, katika sera za kinidhamu nchini Marekani, watoto Weusi wana uwezekano wa karibu mara nne zaidi wa kusimamishwa shule kuliko watoto wa kizungu, na zaidi ya mara mbili ya uwezekano wa kukamatwa kutokana na makosa mbalimbali shuleni, imeeleza ripoti hiyo.

Ripoti pia imeonesha utofauti mkubwa kati ya makabila madogo na jamii za asili.

Kwa mfano, nchini Lao, asilimia 59 ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 kutoka kabila la Wamon-Khmer walio wachache wameandikishwa wakati wa kuzaliwa, wakati wale wa kabila la Lao-Tai waliowengi waliaondikishwa ni asilimia 80. Usajili wa watoto wakati wa kuzaliwa ni muhimu kwakuwa ni sharti la kupata haki za kimsingi kwa taifa.