UNICEF:Walichopoteza watoto kielimu kutokana na COVID-19 ni vigumu kurekebishika

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF limesema kiwango cha hasara wanayopata watoto kielimu kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa elimu kulikosababishwa na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 ni vigumu kurekebishika.

Taarifa ya UNICEF  iliyotolewa leo jijini New York, Marekani inasema kuvurugika kwa mfumo wa utoaji elimu iwe kwa shule kufungwa kabisa au mchanganyiko wa kusomea nyumbani na mtandaoni kumeathiri zaidi ya watoto milioni 635 duniani kote.

Ikiwa ni takribani miaka miwili tangu kuanza kwa janga la COVID-19,  UNICEF inatoa takwimu  hizo hii leo siku ya elimu duniani ambapo mkuu wa masuala ya elimu UNICEF, Robert Jenkins anasema “wakati tunataka kukoma kwa kuvurugwa kwa mfumo wa elimu, kufunguliwa shule pekee hakutoshi. Wanafunzi wanahitaji msaada wa kina ili kufidia kile walichopoteza. Shule lazima ziwe zaidi ya eneo la kujifunza ili kujenga tena afya ya mwili na akili ya mtoto sambamba na maendeleo yake kijamii na kilishe.”

Duniani kote, watoto wamepoteza stadi zao za kuhesabu na kusoma ikimaanisha kuwa mamilioni ya watoto wamekosa mihula yao ya shule ambayo wangalitimiza iwapo wangalikuwa darasani, huku watoto wadogo na walio pembezeno wakipata hasara kubwa zaidi.

Katik anchi za kipato cha chini na kati, kufungwa kwa shule kumesababisha asilimia 70 ya watoto wenye umri wa miaka 10 washindwe kusoma au kuelewa aya rahisi, na kiwango hicho ni ongezeko kutoka asilimia 53 kabla ya COVID-19.

Nchini Ethiopia, wanafunzi wa shule za msingi wanakadiriwa kuwa wangalikuwa wamejifunza kati ya asilimia 30 hadi 40 ya hesabu ambazo wangalijifunza iwapo muhula wa shule ungalikuwa wa kawaida.

Nchini Marekani watoto wameshindwa kujifunza ipasavyo katika majimbo mengi yakiwemo Texas, California, Colorado, Tennessee, North Carolina, Ohio, Virginia na Maryland.

Mathalani huko Texas, mwaka 2021, theluthi mbili ya wanafunzi wa darasa la 3 walipata alama za chini za Hesabu ikilinganishwa na darasa waliloko ikilinganishwa na nusu ya idadi hiyo mwak a2019.

Huko Afrika Kusini, wanafunzi wako nyuma ya muhula wa shule kwa asilimia 75 au muhula mzima ambao walitakiwa kuwa wamesoma. Kati ya mwezi Machi mwaka 2020 na Julai mwaka 2021 watoto wapatao 400,000 hadi 500,000 waliacha shule.

UNICEF inasema pamoja na kupoteza muhula wa masomo, kufungwa kwa shule pia kumeathiri afya ya akili ya watoto, na kupunguza fursa ya kupata lishe bora sambamba na kukumbwa na ukatili.

Watoto wamekumbwa na viwewe na tafiti zinaonesha wasichana na barubaru walioko vijijini wako hatarini zaidi kupata shida hizo. Zaidi ya Watoto milioni 370 walikosa mlo shuleni, ikimaanisha walipoteza chanzo cha mlo bora na wa uhakika,imesema UNICEF.