Mawakili wa utetezi anayewatetea watu 24 wanaokabiliwa na shitaka la mauaji ya askari polisi huko Loliondo, mkoani Arusha nchini Tanzania, wamesema watapeleka maombi mahakamani ili Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) aitwe kujieleza endapo hatakamilisha upelelezi wa kesi hiyo ifikapo Novemba 22 mwaka huu.
Watuhumiwa hao wamekuwa rumande tangu walipokamatwa na kushtakiwa Juni 16, 2022 wakidaiwa kumuua askari polisi Koplo Garlus Mwita kufuatia mapigano kati ya wakazi wa eneo hilo na askari waliokuwa wakishiriki shughuli ya kuweka mipaka eneo la Pori Tengefu la Loliondo.
Watuhumiwa wanaoshtakiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer, madiwani 10 wa chama hicho pamoja na wananchi wa kawaida.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilipanga kutaja kesi hiyo leo Novemba 8, 2022 lakini Wakili wa Serikali Upendo Shemkole aliimweleza Hakimu Mkazi, Harieth Mhenga kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
“Kuhusiana na hoja zilizoongelewa nyakati zilizopita pamoja na amri ya mahakama hii nimezifikisha mahali husika kwa viongozi wa ofisi yetu na zinafanyiwa kazi na tunafuatilia kwa karibu upelelezi ukamilike, hivi karibuni tutaleta majibu mahakamani.Tunaomba tarehe nyingine ya kutaja tukiwa tunasubiri kumalizika kwa upelelezi,” alisemka Shemkole.
Baada ya hoja hiyo, wakili wa utetezi Jebra Kambole alionesha kutoridhishwa na kasi ya upelelezi, akisema hoja ya kutokamilika upelelezi imekuwa endelevu.
“Tumesikiliza hoja za upande wa Serikali, zimekuwa hoja endelevu, siyo mpya. Sisi tunaitaarifu Mahakama hii kwamba tarehe inayofuata kama majibu ni haya, tutaomba mahakama itoe wito kwa RCO Arusha aje hapa aeleze kwa nini hatekelezi maagizo ya mahakama, tunaamini mahakama ina nguvu kisheria ya kumuita mtu yoyote,”alieleza Kambole.
Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Molongo Paschal, Albert Selembo, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Morijoi Parmati, Morongeti Meeki, Kambatai Lulu, Moloimet Yohana na Joel Clemes Lessonu.
Wengine ni Simon Orosikiria,Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, Luka Kursas, Taleng’o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel, Kelvin Shaso Nairoti, Wilson Kiling, James Taki, Simon Saitoti na Joseph Lukumay.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mawili likiwemo la kula njama ya kuua maafisa wa Serikali na maafisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka Pori Tengefu la Loliondo.
Inadaiwa katika kosa la pili kuwa Juni 10, 2022, katika eneo la Ololosokwan, Wilaya ya Ngorongoro, kwa nia ovu, walisababisha kifo G 4200 Koplo Garlus Mwita.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 22, 2022 itakapotajwa tena.