Upinzani wa Tanzania wapinga wagombea wao kuzuiliwa kushiriki uchaguzi ujao

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema, Freeman Mbowe, akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, kimeilalamikia mamlaka nchini humo kwamba wagombea wake wengi wamekataliwa “kwa njia isiyo ya haki” kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo. 

Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi katika miji na vijiji kote nchini tarehe 27 Novemba, uchaguzi ambao unatarajiwa kuwa kipimo cha hali ya kisiasa kabla ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka ujao. 

Uchaguzi huu utakuwa mtihani wa kwanza kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alichukua madaraka baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake, Rais John Magufuli, mwaka 2021. Alianza kutambulika kwa kupunguza vikwazo vilivyokuwa vimewekwa na Magufuli dhidi ya upinzani na vyombo vya habari katika nchi yenye takriban watu milioni 67. 

Hata hivyo, mashirika ya haki za binadamu na serikali za Magharibi zimekiri kile wanachokiita kurejea kwa ukandamizaji kuelekea uchaguzi, huku kukiwa na kukamatwa kwa wanasiasa wa Chadema, pamoja na kutekwa na mauaji ya viongozi wa upinzani.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama hicho kilipanga kuwasimamisha wagombea kwa asilimia 65 ya nafasi 80,430 zinazoshindaniwa, lakini sasa kimepangwa kushiriki kwa takriban asilimia 33 tu. 

“Tumeona kufutwa kwa wagombea wetu kwa ukiukwaji wazi wa taratibu… ilikuwa ni hila ya makusudi,” Mbowe aliwaambia waandishi wa habari. Alisema wengi walizuiliwa kwa kile alichokiita makosa madogo ya kiutawala kama vile kukosa mihuri, makosa ya majina au jinsi fomu za uteuzi zilivyokamilishwa. 

Chadema kilisusia uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 chini ya Magufuli, pia kwa kutilia shaka ukiukwaji wa taratibu za uteuzi. 

“Safari hii, hatuwezi kamwe. Tutasonga mbele hadi mwisho,” alisema Mbowe. “Katika miaka mitano iliyopita, hatujakuwa na uongozi wa msingi. Hatuwezi kubaki nje tena.”

Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  alisema kuwa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesimamisha wagombea kwa nafasi zote zinazoshindaniwa. 

Alisema vyama vya upinzani vimepata uteuzi wa asilimia 38, akielezea maandalizi ya uchaguzi kama “mafanikio na somo la muhimu kwa uchaguzi ujao.”

“Huu ni uchaguzi wa kwanza unaozungumziwa kwa upana na makundi yote ya kijamii,” alisema, akiongeza kuwa Watanzania milioni 31 wamesajiliwa kupiga kura. “Natumai Watanzania wataendelea na mjadala huu, kwani unatujenga kuhusu umuhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika kuimarisha demokrasia yetu.”

Lakini viongozi wa kidini pia wamekosoa mchakato wa uteuzi. 

“Tunasisitiza kwamba wasimamizi wa uchaguzi wafanye majukumu yao kwa usawa, bila kufuata chama chochote cha kisiasa. Kukiuka mapenzi ya wananchi kunasababisha viongozi ambao siyo chaguo lao halisi,” alisema Wolfgang Pisa, rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania. 

“Uadilifu ni kipengele muhimu cha uchaguzi na bila yake, tunajihatarisha kuvuruga amani,” aliongeza Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania, Nuhu Mruma.