Search
Close this search box.
Africa
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ally Mwinyi

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ally Mwinyi amesema licha ya upotoshwa unaofanywa na baadhi ya watu kuhusu serikali yake kamwe hatoprudi nyuma katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar

Rais Mwinyi alisema baada ya serikali kuingia makubaliano na kampuni ya kimataifa ya Dnata kuendeshwa uwanja wa ndege kisasa, yamekuwapo maneno mengi ya upotoshaji.

Alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar na kutoa ufafanuzi wa hoja saba kuhusu kasumba na upotoshaji wa taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii.

Alisema pia kuna upotoshwaji wa taarifa kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayojengwa ikiwamo masoko, viwanja vya michezo vya kisasa ambayo serikali imeingia ubia na sekta binafsi katika kujenga miradi hiyo.

Alisema Zanzibar inategemea utalii na utalii unaanzia kwenye uwanja wa ndege, hivyo zinahitajika kampuni kubwa zenye kutoa huduma za kisasa.

“Yote wanayosema na waseme maana ni uzushi mtupu lakini sirudi nyuma hata hatua moja, ukweli ndio huu kwamba nina nia njema na wananchi wa Zanzibar na ndio maana ninafanya maendeleo,” alisema.

Aidha alisema kuna taarifa za upotoshajwi kuhusu ukodishwaji wa visiwa 10 vilivyokodishwa na serikali yake na kusisitiza kuwa serikali ya awamu ya nane siyo iliyoanza ukodishwaji wa visiwa.

Alisema siyo jambo geni wala la aibu kukodishwa visiwa hivyo ambapo baadhi ya visiwa vilikodishwa miaka 30 iliyopita.

Dk. Mwinyi alisema kuwa visiwa 10 vilivyokodishwa na serikali yake, vitakuza sekta ya utalii na serikali kupata mapato ambapo zaidi ya dola milioni 440 zitapatikana kwa ukodishwaji wa visiwa hivyo.

“Serikali ina dhamira njema ya kuleta maendeleo na ndio maana tumewekeza katika kuvikodisha visiwa vidogo 52 vilivyopo Zanzibar na hadi sasa tumeshakodisha visiwa 10 na wala visiwa havijauzwa kama baadhi ya watu wanaosambaza taarifa za uzushi katika mitandao ya kijamii,” alisema.

Rais Dk. Mwinyi alisema uwekezaji mdogo uliokuwa ukifanywa katika visiwa hivyo hausaidii nchi kwa sababu kodi inayopatikana ni ndogo na watalii wachache kufika huko.

Alisema miaka ya nyuma serikali ilikuwa ikikodisha visiwa  kwa Dola 1,000 kwa mwaka, jambo ambalo haliipatii pato serikali na uwekezaji wa sasa ni mkubwa, akitolea mfano kisiwa kimoja cha Kwale kimekodishwa kwa dola milioni 80 kwa mwaka.

Alisema kuwa hakukuwa na usiri katika ukodishwaji wa visiwa hivyo na zabuni ilitangazwa na taratibu zikafuatwa hadi kuwapata wawekezaji waliokodi visiwa hivyo.

Akizungumzia demokrasia, Dk. Mwinyi alisema demokrasia ya CCM ni nzuri na haitoi nafasi ya uongozi kwa uenyeji bali inafuata katiba, kanuni na maadili.

Kuhusu kauli iliyotolewa na aliyekuwa mwasiasa mkongwe Zanzibar, Baraka Shamte, kwamba akimaliza muda wake wa miaka mitano apishe wengine, alisema wananchi ndio watakaompima kutokana na utendaji wake.

Alipoulizwa kuhusu suala la kumsamehe Shamte kutokana na matashi yake kama ambavyo aliomba radhi mwenyewe kupitia mitandao ya kijamii, Dk. Mwinyi alisema msamaha huo haujazingatia taratibu za kumwomba msamaha.

“Baraka amejikita zaidi kuomba radhi kwa chama chake cha CCM kuwa arejeshwe CCM na wala hajaniomba radhi mimi binafsi kutokana na alivyonikashifu,” alisisitiza Dk. Mwinyi.

Comments are closed