Urusi inasema “kuna maendeleo mazuri” katika mazungumzo na Ukraine

Mawaziri wa Ukraine na Urusi katika mazungumzo yaliyofanyika mjini Belarus mnamo machi 7 2022. (Photo by Maxim GUCHEK / BELTA / AFP) / Belarus OUT

Urusi ilisema Jumatano kwamba mazungumzo na Kyiv kusuluhisha mzozo wake na Ukraine yanaendelea na kusisitiza kuwa wanajeshi wa Moscow hawakuwa na nia ya kuiangusha serikali ya Ukraine.

“Mafanikio machache yamepatikana,” msemaji wa wizara ya mambo ya nje Maria Zakharova alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari, akizungumzi awamu tatu za mazungumzo na Kyiv.

Maafisa wa Ukraine na Urusi wamekuwa wakikutana kwenye mpaka wa Belarus na Poland kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Zakharova alisema duru nyingine ya mazungumzo italenga njia salama za kuwaondoa raia.

Pia alisema Moscow haina nia ya kuiteka Ukraine au kupindua serikali yake.

Lengo la jeshi “sio kuiteka Ukraine, au kupindua serikali. Mzozo hauelekezwi dhidi ya raia,” Zakharova alisema.

Rais Vladmir Putin amesema alituma wanajeshi wake nchini Ukraine ili “kumaliza uongzi wa kinazi” nchi humo.

Tangu wanajeshi wa Urusi walipoingia nchini humo Februari 24, wameshambulia kwa makombora miji mikuu ya Ukraine, na kuwalazimu maelfu kukimbia.

Moscow inasema haijalenga maeneo ya kiraia, licha ya habari zinazoenea.

Wakati wa mkutano huo Zakharova alishutumu mamlaka ya Kyiv kwa kuzuia juhudi za kuwahamisha raia.

“Taarifa kuhusu njia salama kwa binadamu hazijawasilishwa kwa makusudi kwa watu,” alisema.

“Watu wanaotaka kuondoka kwenda Urusi wanalazimika kuhama kuelekea Magharibi,” alisema.

Urusi na Ukraine zimekubaliana kusitisha mapigano kwa siku moja Jumatano katika maeneo ya uokoaji ili kuruhusu raia kutoroka mapigano.

Moscow ilisema wiki hii itaweka njia za uokoaji, lakini Kyiv ilisema njia zilizopendekezwa hazikubaliki kwa sababu zingine zinaelekea Urusi.

Zakharova alidai kuwa karibu watu milioni mbili wa Ukraine wanataka kuhamishwa kuenda Urusi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limekadiria jumla ya wakimbizi wa Ukraine milioni 2.2 wametoroka nchi yao.