Idara ya usalama ya FSB ya Urusi leo imesema kwamba Ukraine ndiyo iliyohusika na shambulio la bomu kwenye gari katika viunga vya mji wa Moscow na kumuua binti wa mwana itikadi kali wa Urusi Alexander Dugin.
Dugin msomi aliye na msimamo mkali na mfuasi mkubwa wa mashambulizi ya Kremlin nchini Ukraine anafikiriwa kuwa ndiye aliyelengwa na shambulio hilo.
“Uhalifu huo ulitayarishwa na kufanywa na huduma maalum za Ukraine,” FSB ilisema katika taarifa iliyobebwa na mashirika ya habari ya Urusi.
Iliongeza kuwa mhalifu ni mwanamke na raia wa Kiukreni aliyezaliwa mwaka 1979.
FSB katika taarifa yake ilimtambua mwanamke huyo kama Natalia Vovk.
Daria Dugina aliuawa siku ya Jumamosi wakati bomu lililowekwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lilipolipuka alipokuwa akiendesha barabara kuu yapata kilomita 40 (maili 25) nje ya Moscow.
Kulingana na taarifa ya FSB, mshambuliaji huyo alifika Urusi mnamo Julai 2022 na binti yake wa umri mdogo na akakodisha nyumba katika jengo moja ambalo Dugina aliishi.
Aliyedhaniwa kuwa mshambuliaji alimfuata Dugina akiwa kwenye Mini Cooper yenye sahani za usajili zilizotolewa Kazakhstan, Ukraine na katika Jamhuri ya Watu wa Donetsk iliyojitenga mashariki mwa Ukraine, FSB iliongeza.
FSB ilisema mshambuliaji huyo alikuwa kwenye tamasha nje ya Moscow ambayo Dugin na binti yake walihudhuria siku ya Jumamosi.
Ripoti kutoka vyombo vya habari vya Urusi zilipendekeza Dugina aliazima gari la babake dakika za mwisho.
Dugin, 60, wakati mwingine huitwa “Putin’s Rasputin” au “Ubongo wa Putin,” ni msomi wa Kirusi aliye na msimamo mkali sana.
Kwa muda mrefu ametetea kuunganishwa kwa maeneo yanayozungumza Kirusi katika himaya mpya kubwa ya Kirusi na aliunga mkono kwa moyo wote operesheni ya Moscow nchini Ukraine.
Aliwekwa kwenye orodha ya vikwazo vya Magharibi baada ya Urusi kutwaa Crimea mwaka 2014, hatua ambayo pia aliunga mkono.
Mshauri wa rais wa Ukraine, Mykhaylo Podolyak, Jumapili alikanusha kuwa mamlaka ya Kyiv ndiyo iliyohusika na shambulio hilo.