Urusi yashambulia ghala la silaha za Ukraine.

Wizara ya ulinzi ya Urusi leo imesema vikosi vya nchi hiyo vimelishambulia ghala la silaha la Ukraine kwenye viunga vya mji wa Rivne na kuliharibu pamoja na vifaa vingine vya kijeshi. 

Wizara hiyo imesema imeshambulia ghala hilo kwa kutumia makombora ya masafa marefu yaliyorushwa kutoka baharini. 

Wakati huo huo, viongozi wa Ukraine wameishutumu Urusi kwa kuwakamata wafanyakazi 15 wa uokozi na madereva wa malori ya msaada wa kiutu wanaojaribu kupeleka chakula na vifaa vingine kwenye mji wa Mariupol.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky anakadiria kuwa raia 100,000 wamebakia Mariupol mji ambao umekuwa ukishambuliwa na askari wa Urusi kwa wiki kadhaa. 

Jana Zelensky alivishutumu vikosi vya Urusi kwa kuizuia misafara ya misaada ya kiutu, licha ya kuwepo makubaliano ya kuruhusu njia za kiutu ili kuwaondoa raia.