Ushiriki mdogo wa wapiga kura wakati Tanzania inapiga kura bila upinzani

Idadi ndogo ya wapiga kura imeonekana katika vituo vya kupigia kura jijini Dar es Salaam leo Jumatano, wakati ambapo wapinzani wakuu wa Rais Samia Suluhu Hassan wengine wakiwa gerezani na wengine wamezuiwa kugombea.

Serikali na polisi walitoa vitisho kadhaa wakisema maandamano hayatavumiliwa, na walipanga magari ya kivita katika jiji hilo la kibiashara siku ya Jumatano ili kuzuia machafuko yoyote.

Hata hivyo, ulinzi huo mkali huenda umeleta athari tofauti, kwani wapiga kura wengi waliogopa kujitokeza kupiga kura.

Waandishi wa habari walishuhudia vituo vingi katika maeneo yenye shughuli nyingi jijini humo vikiwa tupu saa moja baada ya kufunguliwa, kinyume na chaguzi zilizopita ambapo wakati kama huo kulikuwa na misururu mirefu ya wapiga kura.

“Tutawahamasisha watu kutoka mitaani na majumbani mwao waje kupiga kura,” alisema afisa mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, akiomba jina lake lisitajwe.Tunapaswa kuokoa hali hii kwa sababu wengine wanahofia kujitokeza,” aliongeza.

Mfanyabiashara wa chakula, aliyejitambulisha kwa jina moja tu Saada, mwenye umri wa miaka 40, alisema anaogopa kupiga kura kwa sababu ya hofu ya vurugu

Shirika la Amnesty International limelaani kile ilichokiita “wimbi la hofu” kabla ya uchaguzi, likitaja “kutoweka kwa watu, mateso, na mauaji ya kiholela dhidi ya wanachama wa upinzani na wanaharakati.”

Rais Hassan, mwenye umri wa miaka 65, anatarajiwa kuimarisha nafasi yake kupitia ushindi mkubwa utakaonyamazisha wakosoaji ndani ya chama chake, kwa mujibu wa wachambuzi.

Mpinzani wake mkuu, Tundu Lissu, anakabiliwa na kesi ya uhaini na huenda akahukumiwa kifo. Chama chake, Chadema, kimezuiwa kushiriki uchaguzi.
Mgombea mwingine Luhaga Mpina wa ACT-Wazalendo, azuiwa kufanya uchaguzi kutokana na kile kilichoitwa kulikuwa na dosari katika mchakato wa yeye kugombea nafasi hiyo kupitia chama chake.

Hassan alipandishwa madaraka kutoka Makamu wa Rais mwaka 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, aliyekuwa na utawala wa kiimla.

Awali, alisifiwa na watetezi wa demokrasia kwa kulegeza vizuizi dhidi ya upinzani na vyombo vya habari, lakini matumaini hayo hayakudumu.

Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa “serikali imekandamiza wapinzani wa kisiasa na wakosoaji wa chama tawala, imedhibiti vyombo vya habari, na imeshindwa kuhakikisha uhuru wa tume ya uchaguzi.”

Kuna hofu kuwa hata baadhi ya wanachama wa chama tawala wanashambuliwa.
Humphrey Polepole, msemaji wa zamani wa CCM na balozi wa zamani nchini Cuba, alipotea mwezi huu baada ya kujiuzulu na kumkosoa Rais Hassan.Familia yake iligundua mabaki ya damu nyumbani kwake.

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimesema kemerekodi matukio 83 ya utekaji tangu Hassan aingie madarakani, huku mengine 20 yakiripotiwa wiki za karibuni.