Search
Close this search box.
Africa

Serikali ya Tanzania imesema sababu za wananchi nchini humo kujichukulia hatua mkononi ni wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, ulevi na imani za kishirikini.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na  Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Hassan Chande, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya swali lilioulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso ambaye ametaka kufahamu nini kauli ya Serikali katika kutatua changamoto ya wimbi kubwa la mauaji nchini Tanzania.

“Matukio mengi yanasababishwa na wananchi kujichukulia sheria mkononi, wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, ulevi na imani za kishirikina,”amesema.

Amesema katika kudhibiti wimbi hili waliunda timu maalum ya kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.

Chande amesema pamoja na kuchukua hatua za kisheria kama zilivyopendekewa na timu waliyoiunda, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kutoa elimu kwa wananchi.

Amesema elimu hiyo imekuwa ikitolewa  kwa kuwashirikisha viongozi wa siasa, dini, wazee wa mila na watu wanaoheshimika kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, katika kutatua migogoro na migongano katika jamii.

Baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema licha ya Serikali kuchukua hatua bado wimbi la mauaji linaendelea kukua

“Sasa sijui kwamba ni kwasababu polisi ndio wanaoviambia vyombo vya habari, kwa hiyo inakuwa ni habari nzito fulani. Hivi mwingine ambaye anajua kuwa hilo jambo haliwezekani anafikiri kuwa na mimi naweza kulifanya,”amesema.

Spika ameitaka Serikali kuangalia hatua za kawaida na kwamba pengine matangazo nayo yanaleta hiyo changamoto.

“Na mtuulize sisi watu wa kawaida kabisa tunafikiri hilo jambo linaweza kumalizwa kwa namna gani kwasababu kadri linavyozungumzwa utasikia leo huku, kesho huku, sasa huenda linatembea kwasababu linazungumzwa na watu wazito,”amesema.

Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge George Simbachawene amesema iko haja ya kushirikiana na wadau wote katika kukabiliana na changamoto hiyo.

“Law enforcers (wasimamizi wa sheria), tujiulize tunatimiza wajibu wetu sawa sawa, kama kunatokea hasira ya wananchi kuchukua hatua mkononi kwanini wanachukua hatua mkononi? Ni wapi hapako sawa,”amesema.

Comments are closed