UTAFITI: Dar kinara kwa kiwango cha mimba kuharibika

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 uliofanywa kwa ushirikiano na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara za Afya Tanzania Bara na Zanzibar,  umeonesha Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kiwango cha kuharibika mimba.

Utafiti huo ulilenga kutoa takwimu za kufuatilia na kutathmini hali ya afya ya watu nchini. 

Huo ni utafiti wa saba katika mfululizo wa utafiti wa kitaifa wa kidemografia na afya uliowahi kufanyika Tanzania mwaka 1991/92 ambapo kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, taarifa za ujauzito kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya utafiti huo, zimeonesha asilimia 90 walizaa watoto hai na asilimia 10 walipoteza ujauzito. 

Utafiti umeonesha kuwa kati ya wanawake waliopoteza ujauzito, asilimia nane ya mimba zao ziliharibika, asilimia mbili walizaa watoto wafu na asilimia chini ya moja walitoa mimba. 

 “Asilimia 23 ya mimba katika Mkoa wa Dar es Salaam ziliharibika, hiki ni kiwango kikubwa kuliko mkoa wowote na kiwango cha chini zaidi (chini ya asilimia moja) kilikuwa Mkoa wa Rukwa,” imeeleza taarifa ya matokeo ya utafiti huo.

 Utafiti umeonesha kuwa asilimia 22 ya vijana wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wamewahi kupata ujauzito, asilimia 16 walijifungua, asilimia sita walikuwa wajawazito katika kipindi cha utafiti, asilimia mbili waliwahi kuharibikiwa mimba.