Search
Close this search box.
Africa

Matokeo ya utafiti mpya wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani na masuala ya afya ya uzazi UNFPA yaliyotolewa Julai 5,2022  yanaonesha kuwa karibu theluthi moja ya wanawake wote katika nchi zinazoendelea wanaanza kupata Watoto wakiwa na umri wa miaka 19 au chini ya hapo, na karibu nusu ya uzazi wote wa mara ya kwanza wa barubaru huwa ni wa Watoto au wasichana wa umri wa miaka 17 au chini ya hapo. 

Ingawa uzazi umepungua kote ulimwenguni, ripoti hiyo ya UNFPA inaonesha kuwa wanawake ambao walianza kujifungua katika umri wa barubaru walikuwa na karibu watoto 5 walipofikisha umri wa miaka 40 kati ya mwaka 2015-2019.

Mkurugenzi mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem amesema “Wakati karibu theluthi moja ya wanawake wote katika nchi zinazoendelea wanakuwa akina mama wakati wa ujana, ni wazi kuwa dunia inawaangusha wasichana. Mimba za kurudia tunazoziona miongoni mwa wasichana ni ishara tosha kwamba wanahitaji sana taarifa na huduma za afya ya uzazi.”

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo baada ya kupata mtoto wao wa kwanza, kuongeza idadi ya watoto kwa wasichana vigori imekuwa ni kawaida.  

Miongoni mwa wasichana waliojifungua kwa mara ya kwanza wakiwa na umri wa miaka 14 au chini, karibu robo tatu yao pia huzaa mara ya pili wangali vigori na asilimia 40 ya wale walio na watoto wawili huendelea hadi kuzaa mtoto wa tatu kabla ya kuondoka kwenye ubarubaru. 

Utafiti pia umeonya kwamba matatizo yanayotokana na kujifungua ndiyo chanzo kikuu cha vifo na majeraha kwa wasichana barubaru, lakini kuwa mama kigori kunaweza kusababisha ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki zao za kibinadamu na madhara makubwa ya kijamii, ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kingono na masuala ya afya ya akili.  

Umeongeza kuwa akina mama vigori ndio wanaokabiliwa na hatari kubwa zaidi. 

Hata hivyo umatokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa kote duniani, kuna dalili za kutia moyo za kupungua kwa viwango vya uzazi katika umri wa utoto na ujana, lakini kasi ya kupungua huko imekuwa polepole sana mara nyingi kwa takriban asilimia tatu kwa kila muongo.

Dkt. Kanem amesisitiza kuwa “Serikali zinahitaji kuwekeza kwa wasichana barubaru na kusaidia kupanua wigo wa fursa zao, rasilimali, na ujuzi, na hivyo kusaidia kuepuka mimba za mapema na zisizotarajiwa. Wasichana wanapoweza kupanga maisha yao wenyewe, uzazi katika umri mdogo utakua nadra sana.” 

Ripoti hiyo imetoa mapendekezo kwa watunga sera ikiwa ni pamoja na hitaji la kuwapa wasichana elimu ya kina ya kujamiiana na afya ya uzazi, ushauri, usaidizi wa kijamii, na huduma bora za afya, kutoa msaada wa kiuchumi kwa familia, na kushirikisha mashirika ya ndani, yote yakiwa ndani ya sera inayounga mkono na mfumo wa kisheria unaotambua haki, uwezo na mahitaji ya vijana, hasa wasichana barubaru waliotengwa. 

Comments are closed