Utafiti mpya uliochapishwa Oktoba 17,2023 katika jarida la kisayansi la kimataifa la Sage, umeonesha kuwa wagonjwa wa moyo waliowekewa betri ya moyo wamepata hatari ya kukumbwa na changamoto ya akili.
Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ulihusisha wagonjwa sita ambao wamewekewa betri hiyo baada ya kufanyiwa vipimo vya mtambo mkubwa uitwao CathLab.
Mkuu wa Idara ya Utafiti wa JKCI, Dk Pedro Pallangyo , amesema utafiti huo ulilenga kuangaliwa wale ambao wanafanyiwa uchunguzi wa moyo wanaoingia katika mshine ya cathlab, ambao wamewekewa betri ya moyo, ambapo wanafatilia maisha yao yamekuwaje baada ya kuwekewa vifaa hicho.
“Tumegundua kwamba kesi za wagonjwa sita ambao wote wamewekewa betri za moyo baada ya kuwekewa waliweza kupata changamoto ya afya ya akili kwa maana kwamba walikuwa hawajajiandaa kupokea kuwekewa vifaa vya kusaidia moyo na badala yake wote sita wakawa na dalili za magonjwa ya mfumo wa akili,”alieleza.
Alifafanua kuwa baada ya kugundua hilo waliwatafuta mabingwa wa mfumo wa akili, ili kuweza kutibu tatizo hilo.
Aidha ameeleza kuwa tafiti zingine duniani zimeonesha kwamba wagonjwa wanaowekewa vifaa hivyo pia lazima waendelee na matibabu mengine, hivyo wasipotambulika mapema na kutibiwa wana uwezekano mkubwa wa kutozingatia ushauri wa kiafya waliopewa kuanzia upande wa kubadilisha mfumo wa maisha na uzingatiaji wa dawa.
Dk Pallangyo amesema utafiti huo unalenga kuwaamsha jamii hasa ya watoa huduma kama madaktari na wauguzi kuwa makini na kuhakikisha wagonjwa wao wote kabla ya kuwekewa hivyo vau kufanyiwa upasuaji kwa ujumla au baada ya kufanyiwa upasuaji wanahakikisha wanaangalia kwanza mfumo wa akili au afya ya akili.
“ Wanaangalia hayo ili kuweza kuingilia kati kwa maana ya matibabu pale inapobidi kwa maana wagonjwa hao wasipogundulika mapema wanaweza kupoteza maisha,”alisisitiza.
Dk Pallangyo amesema kisa kingine kilichotokea hivi karibuni ni mtu mmoja ambaye aliwekewa betri ya moyo na akajirusha kutoka ghorofani na kufariki, hali hiyo ni kutokana na mfumo wake wa akili kutojikubali na kuathiri afya ya akili baada ya kuwekewa hizo betri.