Jeshi la Polisi nchini Tanzania linawashikilia viongozi wakuu wa chama cha upinzani cha Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, aliyekuwa mgombea urais Tundu Lissu, na kuwakusanya mamia ya wafuasi wa vijana wa chama hicho
Viongozi hao wa Chadema walikamatwa Kusini Magharibi mwa jiji la Mbeya, ambako chama hicho kilipaswa kufanya mkutano leo Jumatatu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana.
Watu wapatao zaidi ya 300 wamekamatwa na polisi walipokuwa wakielekea Mbeya na kurudishwa nyumbani.
Polisi wa Tanzania walikuwa wametangaza Jumapili kupiga marufuku mkusanyiko wa vijana wa Chadema, wakishutumu chama hicho kwa kupanga maandamano yenye vurugu.
Umoja huo wa vijana umesema takribani vijana 10,000 walikuwa wanatarajiwa kukutana jijini Mbeya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana chini ya kauli mbiu ya “Chukua mustakabali wako”.
Tangu achukue usukani mwaka 2021 baada ya kifo cha ghafla cha Rais John Magufuli, Rais Samia ameachana na sera za kimabavu za mtangulizi wake na kuanza mageuzi ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kulegeza vikwazo kwa vyombo vya habari na upinzani.
Mnamo Januari 2023, aliondoa marufuku dhidi ya mikutano ya upinzani iliyowekwa mnamo 2016 na Magufuli, katika harakati za wapinzani wa kisiasa wanaotaka kurejeshwa kwa mila za kidemokrasia.
Lissu alikuwa amerejea Tanzania mara baada ya Rais Samia kuondoa marufuku hiyo, na hivyo kuhitimisha miaka mitano aliyokaa uhamishoni kufuatia jaribio la kutaka kumuua mwaka 2017.
Machi 2022, Mbowe aliachiliwa takriban miezi saba baada ya yeye na viongozi wengine wa Chadema kukamatwa saa chache kabla ya chama hicho kufanya kongamano la kudai marekebisho ya katiba.
Akitangaza marufuku hiyo siku ya Jumapili, Awadh Haji, Mkuu wa Polisi wa Tanzania anayesimamia operesheni na mafunzo, alisema jeshi hilo lina dalili za wazi kuwa lengo lao si kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Vijana bali kuanzisha na kushiriki katika vurugu.
Lissu aliapa siku ya Jumapili kuwa shughuli hiyo ya vijana ingeendelea kama ilivyopangwa.
“Rais Samia usilete mambo ya ajabu ya Magufuli, Siku ya Vijana Duniani inaadhimishwa duniani. Kwanini polisi wako wanawazuia vijana wa Chadema barabarani na kuwakamata?” Alisema kwenye X.
“Huu sio wakati wa kukaa kimya, kuogopa, au kuzungumza tu. Ni wakati wa kusimama na kuhesabiwa. Tupaze sauti zetu kwa nguvu zetu zote!”
– Wanaharakati walaani
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeungana na wadau wengine wa Haki za Binadamu nchini Tanzania kulaani tukio la kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA na waandishi wa habari waliokuwa wakielekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana duniani jijini Mbeya
Taarifa iliyotolewa leo na THRDC imeeleza kuwa zaidi ya watu 300 wamekamatwa na Jeshi la Polisi akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi(SUGU).
Katika nyakati tofauti tofauti mnamo Agosti 11, 2024 makundi hayo ya vijana na viongozi wao waliokuwa wakisafiri kwenda jijini Mbeya kwaajili ya maadhimisho ya siku ya vijana duniani ambayo yalipangwa kufanyika leo jijini Mbeya chini ya mwavuli wa Baraza la Vijana Chadema walikamatwa ndani ya magari yao waliyokuwa wamekodi na kufanyiwa upekuzi katika maeneo ya Mikese Morogoro (takribani watu 80), Iringa (takribani watu 90), Makambako (takribani watu 70) na Mbeya (takribani watu 100), idadi hii ya watu ni kwa mujibu wa THRDC
Haya yanajiri ikiwa Tanzania inajiandaa kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge mwishoni mwa mwaka ujao.