Polisi katika miji mikuu ya Marekani wanajiandaa kwa ghasia zinazoweza kutokea iwapo rais wa zamani Donald Trump atakamatwa wiki hii kama sehemu ya uchunguzi wa pesa aliyotoa kama rushwa.
Mamlaka huko New York, Washington DC na Los Angeles zinaongeza uwepo wao wa utekelezaji wa sheria.
Mwendesha mashtaka wa Manhattan anaweza kumshtaki Bw Trump kwa madai kwamba alimlipa nyota wa ponografia pesa ili kumnyamazisha asizungumzie uchumba wanaodaiwa kuwa nao.
Itakuwa kesi ya kwanza ya jinai kuletwa dhidi ya rais wa zamani wa Marekani.
Vizuizi vya chuma vilikuwa vinawekwa Jumatatu nje ya Mahakama ya Jinai ya Manhattan, ambapo Bw Trump anaweza kushtakiwa, kuchukuliwa alama za vidole na kupigwa picha iwapo mashtaka yatawasilishwa wiki hii, kama vyombo vya habari vya Marekani vilivyotarajia.
Kuongezeka kwa uwepo wa polisi pia kumeonekana nje ya Mnara wa Trump katika jiji hilo.
Kila mwanachama wa Idara ya Polisi ya New York (NYPD), ikiwa ni pamoja na wapelelezi waliovalia kiraia, wameamriwa kuvaa sare zao kamili siku ya Jumanne na wanawekwa kwenye hali ya kuwa tayari kukabiliana na lolote, chanzo cha polisi kiliiambia CBS, mshirika wa BBC wa Marekani.