Viongozi wa ECOWAS waiondolea Mali vikwazo

Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo akizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ECOWAS wakati wa Kikao cha 61 cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) mjini Accra, Ghana, Julai 3, 2022.. (Photo by Nipah Dennis / AFP)

Viongozi wa Afrika Magharibi siku ya Jumapili waliondoa vikwazo dhidi ya utawala wa kijeshi wa Mali, wakikubali kurejeshwa kwa utawala wa kiraia Machi 2024 na kukubaliana kuruhusu Burkina Faso miaka miwili kwa kipindi cha mpito kurejea demokrasia.

Wakuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wamekutana katika mji mkuu wa Ghana Accra kutathmini juhudi za kupata dhamana ya kurejesha utawala wa kiraia nchini Mali, Guinea na Burkina Faso.

Mali ilifanya mapinduzi Agosti 2020 na Mei 2021, ikifuatiwa na Guinea Septemba 2021 na Burkina Faso Januari hii.

Kwa kuhofia kutokea kwa mapinduzi zaidi katika eneo linalojulikana kwa utekaji wa kijeshi, ECOWAS iliweka vikwazo vikali vya biashara na kiuchumi dhidi ya Mali, lakini adhabu ndogo dhidi ya Guinea na Burkina.

“Baada ya majadiliano, wakuu wa nchi walichukua uamuzi thabiti wa kwanza kuondoa vikwazo vya kiuchumi na kifedha,” Rais wa Tume ya ECOWAS Jean-Claude Kassi Brou aliwaambia waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo kuhusu Mali.

Uamuzi huo pia unadai hakuna mwanajeshi yeyote wa kijeshi anaeryhusiwa kugombea katika uchaguzi ujao wa rais wa Mali, kulingana na mjumbe mmoja wa ECOWAS.

ECOWAS mwezi Januari iliiwekea Mali vikwazo vya kibiashara na kifedha baada ya serikali yake ya kijeshi kuzindua mpango wa kutawala kwa miaka mitano.

Vikwazo hivyo vimeathiri vibaya nchi hiyo ambayo uchumi wake tayari ulikuwa umedorora kutokana na uasi wa muongo mmoja wa wanajihadi.

Baada ya mazungumzo ya miezi kadhaa, mamlaka ya Mali Jumatano iliidhinisha mpango wa kuandaa uchaguzi wa rais mnamo Februari 2024.

Kura hiyo itatanguliwa na kura ya maoni kuhusu katiba iliyorekebishwa Machi 2023 na uchaguzi wa wabunge mwishoni mwa 2023. Mpatanishi wa ECOWAS nchini Mali, kiongozi wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan, alitembelea nchi hiyo wiki iliyopita.

Mjumbe wa msafara wake aliiambia AFP kuwa Mali imepata maendeleo makubwa.

Burkina Faso na Guinea hadi sasa zimesimamishwa kutoka kwa shughuli za jumuiya hiyo ya mataifa 15.

Serikali ya Burkina ilipendekeza kura ya maoni ya kikatiba mnamo Desemba 2024 na uchaguzi wa urais mnamo Februari 2025. Mjumbe wa ECOWAS alisema wakuu wa nchi wa kanda walikubaliana na ratiba ya miaka miwili ya mpito.

Taarifa hizo zilithibitishwa kwa AFP na afisa wa ECOWAS ambaye pia alishiriki katika mkutano huo.

Akizuru Ouagadougou kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja Jumamosi, mpatanishi wa ECOWAS Mahamadou Issoufou alikuwa amemsifu kiongozi wa kijeshi Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba na serikali yake kwa ‘uwazi wao wa mazungumzo.’

Ratiba ya kurejea kwa utawala wa kiraia na hali ya kiongozi aliyeondolewa madarakani Roch Marc Christian Kabore pia zilijadiliwa, alisema rais huyo wa zamani wa Niger.

Vyama vya kisiasa vinavyomuunga mkono Kabore vilikashifu mipango ya serikali siku ya Ijumaa, vikisema kuwa havijashauriwa mapema.

Hali inaonekana kuwa ngumu zaidi nchini Guinea, ambayo mamlaka yake imekataa mpatanishi wa ECOWAS na kutangaza kipindi cha mpito cha miezi 36 — kipindi ambacho mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Senegal Macky Sall amekitaja kuwa kirefu sana.

Guinea wiki hii imeongoza mazungumzo ya kidiplomasia ili kupunguza wasiwasi wa viongozi wa kanda.

Waziri mkuu wa nchi hiyo baada ya mapinduzi Mohamed Beavogui siku ya Jumamosi alikutana na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi na Sahel, Mahamat Saleh Annadif.

Serikali ilisema ilitaka kuwahakikishia ndugu zake wa ECOWAS kuhusu kujitolea kwake kufanya mabadiliko ya kidemokrasia ya amani na jumuishi.

Utawala wa kijeshi wa Guinea ulikutana na vyama vikuu vya kisiasa siku ya Jumatatu, lakini wameweka ushiriki wao katika mazungumzo hayo kuwa na masharti ya kuteuliwa kwa mpatanishi wa ECOWAS.