Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Viongozi wa Serikali wadaiwa kuomba rushwa kupitisha posho za walimu - Mwanzo TV

Viongozi wa Serikali wadaiwa kuomba rushwa kupitisha posho za walimu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amekemea vikali tabia ya baadhi viongozi kuomba rushwa ili kupitisha posho za madaraka kwa Walimu Wakuu.

Kairuki ametoa onyo hilo mkoani Kagera wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa elimu na uwekaji wa mpango kazi kwa mwaka 2023.

Amesema kuna baadhi ya Viongozi wa elimu Mkoani na Wilayani wamekuwa na tabia ya kuomba fedha (rushwa) kwa Walimu Wakuu wanapofuatilia vocha za malipo za posho ya madaraka.

“Kumekuwepo na taarifa kuwa baadhi ya viongozi mmekuwa mkiomba fedha kwa walimu wakuu ili muidhinishe fedha zao za posho ya madaraka jambo hili si haki na halikubaliki” amesema Kairuki.

Kutokana na hali hiyo, Kairuki amemuagiza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Dkt. Charles Msonde kuhakikisha fedha za posho za madaraka zinapelekwa moja kwa moja kwenye akauti za benki za wahusika.

“Naibu katibu Mkuu (Dkt. Msonde) tabia hii ikome mara moja, hivyo naagiza muangalie namna ya malipo ya posho za madaraka ya Waalimu Wakuu zipelekwe moja kwa moja kwenye akaunti za wahusika na kuacha kupitisha kwenye mlolongo mrefu ambao unatumika hivi sasa” amesisitiza Kairuki.

Amesema kupeleka fedha kwenye akaunti za wahusika kutapunguza urasimu na michakato mirefu, kuongeza ufanisi na kuwapunguzia walimu mzigo wa kufuatilia fedha.

Aidha, Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaonya Viongozi wenye tabia hizo na kusisitiza kuwa hawatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote watakaobainika kuomba rushwa.