Vitendo vya ukatili vyaongezeka mkoani Katavi

Matukio 270 ya vitendo vya ukatili na unyayasaji wa kijinsia yameripotiwa mkoani Katavi, ukilinganisha na makosa 240 yaliyoripotiwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2021.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ali Makame, amesema makosa hayo yameripotiwa ndani ya miezi tisa kuanzia Januari hadi Septemba 2022.

“Kuna ongezeko la makosa 30 ya ukatili na unyayasaji wa kijinsia, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.5,” alisema. 

Amesema sababu ya matukio kuongezeka ni kupungua kwa utoaji elimu juu ya madhara ya ukatili na unyayasaji wa kijinsia kwa jamii.

Ili kudhibiti matukio hayo, ACP Makame amesema Jeshi la Polisi mkoani humo, limeweka mikakati ya kuongeza kasi ya kutoa elimu, ambayo inaendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari na kupitia njia mbalimbali, ikiwemo mikutano ya hadhara.

Ametoa wito kwa asasi zote, viongozi wa dini na wa serikali na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, kwa kutoa elimu ya madhara ya vitendo hivyo, ili kutengeneza jamii yenye amani.