Wananchi wa Afrika Kusini wanapiga kura katika uchaguzi muhimu zaidi hasa kwa chama tawala cha African National Congress (ANC) tangu mfumo wa ubaguzi wa rangi umalizike nchini humo mwaka 1994.
Zaidi ya wapiga kura milioni 27 wameandikishwa katika uchaguzi ambao haukuwa na uhakika tangu chama cha African National Congress (ANC) kuliongoza taifa hilo kutoka kwa utawala wa kibaguzi — na huku Rais Cyril Ramaphosa akiomba kuchaguliwa tena.
Huku changamoto za upinzani kutoka upande wa kushoto na kulia, ukosefu wa ajira na uhalifu katika viwango vya juu kizazi kipya kinachokua bila kumbukumbu ya mapambano dhidi ya utawala wa watu weupe walio wachache, chama tawala kinaweza kuhitaji kugawana madaraka.
Vyama 70 na wagombea huru 11 wanashiriki katika uchaguzi huo ambao utashuhudia Waafrika Kusini wakipigia kura bunge jipya, na mabunge tisa ya majimbo.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amepiga kura yake ya uchaguzi mkuu leo Jumatano na kusema “hana shaka” kwamba wapiga kura “kwa mara nyingine tena” wataunga mkono chama chake tawala cha African National Congress (ANC).
Baada ya kupiga kura, Ramaphosa alisema: “Sina shaka yoyote katika moyo wangu kwamba watu kwa mara nyingine tena watawekeza imani kwa ANC kuendelea kuongoza nchi hii.
Kikiwa madarakani tangu aliyekuwa mpingaji mkubwa wa ubaguzi wa rangi, Nelson Mandela alipoongoza kwa ushindi mwishoni mwa utawala wa wazungu wachache, ANC kinawania muhula wa saba madarakani.
Ingawa kina uhakika wa ushindi, kura za maoni zimekuwa zikionesha kwamba umaarufu wa chama hicho umepungua, na huenda kitapoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza, na kulazimisha kuingia katika muungano na chama kimoja au zaidi cha upinzani ili kuunda serikali.
Kwa mara ya kwanza, wapiga kura wanapatiwa karatasi tatu za kupigia kura wanakapoingia kwenye chumba cha kupigia kura.
Kura ya kwanza inahusu orodha ya vyama vinavyowania viti 200 vya ubunge nchi nzima.
Kura ya pili inaorodhesha vyama na wagombea huru, katika majimbo yanayowania viti vingine 200 vya ubunge.
Hii ni mara ya kwanza kwa kura hii kuanzishwa ili kuwapa nafasi wagombea huru kugombea ubunge, na kuimarisha uwakilishi wa majimbo katika chombo cha kutunga sheria.
Kwa katiba ya Afrika Kusini, hakuna uchaguzi wa moja kwa moja wa rais. Bunge jipya ndilo litachagua rais, ambaye kwa kawaida ndiye kiongozi wa chama kilicho na wabunge wengi.
Kura ya tatu ni ya mabunge ya majimbo, moja kwa kila majimbo tisa ya Afrika Kusini.
Wapiga kura katika kila jimbo wanapigia kura bunge lao, na safari hii wataweza kupiga kura kwa wagombea huru, badala ya vyama pekee.