Waandaaji watano wa filamu kutoka Afrika Mashariki ni miongoni mwa waaandaji wa filamu 21 kutoka barani Afrika ambao wamepita katika mchujo wa awali wa shindano la shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO pamoja na kampuni ya kutengeneza na kusambaza filamu, Netflix la kutengeneza filamu za hadithi za kiafrika.
Taarifa ya pamoja ya UNESCOna Netflix iliyotolewa leo mjini Paris nchini Ufaransa imesema washindi hao wa awali 21 ni kati ya maombi 2080 yaliyowasilishwa na zaidi ya yote awali washindi walipaswa kuwa 20 lakini kutokana na ubora wa hali ya juu imelazimika kuongeza mshiriki mmoja na hivyo idadi kufikia 21.
Washindi hao ni Walter Mzengi kutoka Tanzania, Loukman Ali wa Uganda, Noni Ireri wa Kenya, Voline Ogutu wa Kenya halikadhalika Oprah Oyugi kutoka Kenya.
Wengine ni Nosa Igbinedion wa Nigeria, Ebot Tanyi wa Cameroon, Tongryang Pantu wa Nigeria, Venance Soro Côte d’Ivoire, Volana Razafimanantsoa wa Madagascar, Mohamed Echkouna wa Mauritania, Nader Fakhry wa Côte d’Ivoire, Anne Catherine Tchokonté wa Cameroon na Mphonyana Mokokwe kutoka Botswana.
Halikadhalika Anita Abada wa Nigeria, Samuel Kanyama Zambia, Machérie Ekwa-Bahango kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Ndiyathemba Modibedi kutoka Afrika Kusini, Gcobisa Yako pia wa Afrika Kusini, Akorede Azeez wa Nigeria, pamoja na Katya Aragão wa São Tomé na Principe.
Sasa washiriki hao 21 katika awamu ya pili wanatakiwa kutengeneza filamu fupi zenye maudhui, Hadithi za Afrika; Fikra mpya na kuwasilisha kazi zao kwa majaji.
Hatma yake ni kupata watengeneza filamu 6 ambao watapatiwa dola 75,000 kupitia kampuni ya uandaaji filamu ili kutengeneza filamu chini ya usimamizi na mwongozo wa Netflix na kisha kila mmoja atapatiwa dola 25,000.