Search
Close this search box.
Africa

Vikosi vya usalama vya Sudan vimewafyatulia mabomu ya machozi  maelfu ya watu waliojitokeza barabarani kutangaza upya matakwa ya utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana.

Waandamanaji walionekana katika mji mkuu Khartoum wakiwa wamebeba bendera za Sudan na kuimba: “Hapana, hapana kwa utawala wa kijeshi,” na “Utawala wa kiraia ni chaguo la watu,” 

Vikosi vya usalama vilifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.

Sudan imekuwa ikikumbwa na maandamano ya karibu kila wiki na ukandamizaji mkali ambao hadi sasa umesababisha takriban watu 116 kuuawa tangu mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan kuongoza mapinduzi ya kijeshi Oktoba iliyopita.

Unyakuzi huo wa madaraka ulisababisha kipindi cha mpito kwa utawala wa kiraia ulioanzishwa baada ya kuondolewa madarakani mwaka 2019 kwa kiongozi shupavu Omar al-Bashir, aliyetawala kwa miongo mitatu.

Sudan imekuwa ikikabiliwa na machafuko ya kisiasa, mzozo wa kiuchumi unaoendelea na kuongezeka kwa mapigano ya kikabila katika maeneo yake ya mbali.

Mwezi uliopita, Burhan aliahidi katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kujiweka kando na kutoa nafasi kwa makundi ya Sudan kukubaliana kuhusu serikali ya kiraia.

Viongozi wa kiraia waliotimuliwa katika mapinduzi hayo walipuuzilia mbali hatua yake na kusema ni “janja”, na waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wameshikilia kwa nguvu kilio chao cha “hakuna mazungumzo, hakuna ushirikiano” na jeshi.

Mapema mwezi huu, naibu wa Burhan na kamanda wa kijeshi Mohamed Hamdan Daglo alikiri kwamba mapinduzi ya Oktoba mwaka jana yameshindwa kuleta mabadiliko nchini Sudan.

“Jambo lote lilishindikana na sasa sisi (Sudan) tumekuwa pabaya zaidi,” alisema.

Mwezi uliopita, kiongozi wa kidini wa Kisufi Al-Tayeb Al-Jed alizindua mpango unaolenga kumaliza mzozo wa kisiasa wa Sudan.

Hatua hiyo ilikaribishwa na Burhan, pamoja na vikundi vya Kiislamu vilivyokuwa sehemu ya utawala wa Bashir.

Comments are closed