Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kutenga maeneo maalum kwa ajili yao na kutoa huduma za tafiti kwa gharama nafuu.
Aidha, amesema serikali itaendelea kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa unafuu ili wachimbaji hao waweze kupata na kuanzisha miradi, na mwishowe waweze kuhitimu na kuwa wachimbaji wakubwa.
Amesema hayo akifunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini Tanzania mwaka 2022, na kusisitiza kwamba, kuimarika kwa sekta ya hiyo ni kukua kwa uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zilizoibuliwa amesema kwamba serikali itazifanyia kazi hata kama itahusisha kubadili sheria, na serikali itakuwa tayari kukutana na kujadiliana na wachimbaji mara kwa mara.
Hata hivyo, amewataka wachimbaji hao kuendelea kuwekeza na kuongeza thamani ya madini nchini, ili Watanzania zaidi wanufaike.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema Wizara inaendelea na jitihada za kumaliza upungufu wa chumvi nchini ambapo uhitaji ni tani laki 2.5, lakini inayozalishwa nchini ni tani laki 1.2.
Aidha, amesema wizara kwa kushirikiana na wadau wengine watahakikisha sekta hiyo inakua na kufikisha asilimia 10 ya mchango wake kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 7.9 ya sasa.