Wafanyabiashara watatu wapandishwa kizimbani kwa kuisababishia TRA hasara ya zaidi ya  shilingi bilioni 10.5

Wafanyabishara watatu wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 13, likiwemo la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzani (TRA)  hasara ya zaidi ya Sh10.5 bilioni.

Washtakiwa hao ni Joseph Msaki(35), Gift Msaki(40) na Constantine Roman(38) ambao ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa serikali wa TRA, Medalakini Godwini alidai watatu hao walitenda makosa hayo kati ya Januari 2018 na Juni 15,2022 jijini Dar es Salaam.

Godwin alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manne ya kukwepa kodi, manne ya kutoa risiti za mashine za EFD zisizo halali, manne ya matumizi yasiyo sahihi ya mashine ya EFD na moja la kuisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh10.5 bilioni

Alidai katika shtaka la kukwepa kodi, washtakiwa kwa pamoja walijihusisha kutoa risiti isiyo halali kwa kutumia mashine ya EFD yenye jina la Romani Shirima ambayo ilikuwa na mauzo ya Sh18.7 bilioni  na hivyo kukwepa  kodi la ongezeko la thamani ya Sh5.6 milioni.

Pia washtakiwa hao wanadaiwa kukwepa kodi kwa kutumia mashine ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Ahmada Ally na kusababisha ukwepaji wa kodi wa Sh784.734 milioni huku mashine hiyo ikifanikisha ukwepaji wa kodi ya Sh 582.6 milioni.

Godwin alidai katika shtaka la kutoa risiti isiyo sahihi katika kipindi hicho washtakiwa hao walitoa risiti isiyo sahihi kwa kutumia  mashine ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Ahmada Ally wakati mashine hiyo ilikuwa na taarifa ya mauzo ya Sh 2.6 bilioni na kusababisha ukwepaji wa  kodi ya Sh784.7 milioni.

Katika shtaka la matumizi yasiyo sahihi ya mashine ya EFD, alidai kati ya Januari 2018 hadi Juni 2022 kwa pamoja, wsashtakiwa walitumia mashine hiyo isiyo sahihi yenye jina la Ngarasoni Shirima ambayo ilikuwa na mauzo ya Sh18.7 bilioni kwa nia ya kumdanganya kamishna mkuu  wa TRA na matokeo yake walikwepa kodi ya ongezeko la thamani  ya Sh5.6 bilioni.

Katika shtaka la kuisababishia TRA hasara, inadaiwa kati ya Januari 2018 hadi Juni 2022 jijini Dar es Salaam wafanyabiashara hao walikwepa kodi na kuisababisha TRA hasara ya Sh10.5 bilioni .