Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Wafaransa wakaribishwa kuja kuwekeza Tanzania - Mwanzo TV

Wafaransa wakaribishwa kuja kuwekeza Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Ufaransa kuja kuwekeza nchini mwake huku akisema serikali ya Tanzania imeboresha mazingira ya kufanya biashara nchini  humo.

Alitoa ukaribisho huo jana jijini Paris nchini Ufaransa wakati  alipohutubia wajumbe wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Ufaransa (MEDEF), Rais Samia amesema kuwa kuna fursa za kuwekeza katika mifugo, kilimo, nishati, madini na sekta nyingine.

“Serikali imefanya mabadiliko makubwa ya kisheria, kitaasisi na kifedha kwenye sekta ya umma kuhakikisha kuna mazingira rahisi ya kuanzisha na kufanya biashara nchini,” alisema Rais Samia.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilieleza kuwa, hatua za serikali yake kuboresha mazingira ya biashara zimeanza kuzaa matunda kwa kuwa mwaka jana kulikuwa na ongezeko kubwa la usajili wa miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI), ambayo  iimesajiliwa  katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Rais Samia alisema mwaka jana TIC ilisajili miradi mipya 256 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.749 inayotarajiwa kutengeneza ajira 53,025.

Ufaransa inashika nafasi ya 35 kwa kiwango cha uwekezaji nchini ikiwa na miradi 40 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 73.4 ambayo hadi sasa imetengeneza ajira 1,885.

Baada ya kuzungumza na wafanyabiashara, Rais Samia alikutana na kuzungumza na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Paris.

Awali Rais Samia alitembelea makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambako alizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Aundrey Axoulay.

Juzi Rais Samia alizungumza na Watanzania wanaoishi Ufaransa akawataka waheshimu sheria za nchi hiyo, wasiharibu sifa ya Tanzania na washirikiane na kusaidiana.

Rais Samia aliondoka wiki iliyopita kwa ajili ya ziara ya kikazi nchini Ufaransa na Ubelgiji.

Wakati huohuo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bouygues Batiment nchini Ufaransa wamesaini makubaliano ya awali (MoU) ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ukarabati wa jengo la pili la abiria (terminal II) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.