Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limetoa tahadhari kwa wananchi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaopanga kufanya mikusanyiko na maandamano ya kuishinikiza Serikali kuachiwa huru Mwenyekiti wa chama hicho Taifa ambaye kesho Aprili 24,2025 atafikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jijini Mwanza leo April 23,2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, imesema Jeshi hilo limepata taarifa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali zinazoonyesha kuwa baadhi ya wafuasi wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, wanapanga kukutana na kufanya mikusanyiko isiyokuwa halali, kwa lengo la kushinikiza kuachiliwa huru kwa Tundu Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
” Kutokana na taarifa hiyo Jeshi la Polisi linawatahadharisha wananchi kutojihusisha au kushiriki katika mikusanyiko hiyo isiyokuwa halali bali linawataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kujipatia kipato bila hofu yoyote,”amesema Mutafungwa
Kwa mjibu wa Kamanda Mutafungwa taarifa hiyo waliyoipata ni kwamba mikusanyiko hiyo itashirikisha wanawake na watoto ambao wanashawishiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kushiriki kwa wingi katika mikusanyiko hiyo isiyokuwa halali.
Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi hilo limeimarisha doria za askari katika maeneo yote ili kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa usalama na amani na wale ambao watajihusisha katika mikusanyiko hiyo isiyokuwa halali, kufanya vurugu au uvunjifu wowote wa amani, Jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kama hatua ya kulinda amani na usalama wa mkoa wa Mwanza.
Hata hivyo Jeshi hilo linawakumbusha wananchi wa mkoa wa Mwanza, kutoa taarifa za mikusanyiko hiyo isiyokuwa halali au uvunjifu wowote wa amani mara moja itakapojitokeza katika maeneo yao ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa na Jeshi la Polisi.