Wafuasi wa CHADEMA wasusia kesi ya uhaini ya Tundu Lissu wakilalamikia manyanyaso ya Polisi

Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakiongozwa na viongozi waandamizi wa chama hicho, wamesusia kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, wakidai kunyanyaswa na kuzuiwa kuingia ndani ya Mahakama Kuu kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.

 

Tukio hilo limetokea leo asubuhi, wakati Lissu alipofikishwa mahakamani kwa ajili ya kuendelea kuwasilisha hoja za kupinga uhalali wa hati ya mashtaka dhidi yake. Hoja hizo alianza kuziwasilisha jana, Septemba 15, 2025.

 

Wafuasi wa CHADEMA walizuiwa kuingia ukumbini, hali iliyosababisha taharuki na hatimaye wafuasi waliokuwa ndani kuamua kutoka kwa pamoja kwa kile walichokiita “kukandamizwa kwa haki ya uwazi na ushiriki wa wananchi katika mashauri ya wazi ya mahakama.”

 

Akizungumza mbele ya jopo la majaji muda mfupi baada ya tukio hilo, Lissu alilalamikia hatua hiyo akisema kuwa amepata taarifa kuwa polisi walitoa agizo la kuwaondoa wafuasi wake waliokuwa ndani ya mahakama.

 

“Katika mazingira ya kawaida nipo tayari kuendelea, lakini watu wametolewa kwa maagizo ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam(ZCO). Polisi wanakataza wananchi kuhudhuria mashauri haya ya wazi. Hii si Mahakama ya Kijeshi, ni Mahakama ya Kiraia, mamlaka ya kuamuru hapa ni ya Majaji pekee,” alisema Lissu.

 

Lissu alisisitiza kuwa kesi hiyo ni ya aina yake na ina umuhimu mkubwa si tu kwa taifa, bali hata kwa jumuiya ya kimataifa inayofuatilia kwa karibu mwenendo wake. 

 

Aliongeza kuwa kitendo cha polisi kuingilia mchakato wa mahakama kinahatarisha uhuru wa mahakama na haki ya mchakato wa kisheria.

 

“Waheshimiwa Majaji, hii ni kesi ya uhaini, hakuna kesi kubwa kama hii. Inafuatiliwa duniani kote. Haiwezekani polisi watoe amri ya watu kuondoka mbele ya majaji. Mkikubali hili, mahakama hii itakuwa kama *Star Chamber Court*, sio ya kiraia,” aliongeza Lissu kwa ukali.

Lissu aliomba mahakama iwaagize watu waliotolewa warudishwe ndani, na shauri hilo liahirishwe hadi hapo watakaporuhusiwa kuhudhuria bila kunyanyaswa.

 

Majaji bado hawajatoa uamuzi kuhusu maombi hayo, ambayo upande wa Jamhuri ulipinga hoja ya Lissu kwa madai kuwa hakuku na mtu aliyezuiwa kuingia ndani ya Mahakama na waliondoka mahakamani baaday ya Majaji kuwasili.

 

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru wameahirisha shauri hilo kwa muda wa saa moja kwa ajili ya kulitolea uamuzi.

 

Endelea kufuatilia kwa taarifa zaidi kadri shauri hili linavyoendelea.