Wafuasi wa mhubiri anayejiita Mfalme Zumaridi, Diana Bundala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, wameendelea kuomba kupewa dhamana, baada ya hapo awali kugomea wakisema wanampa faraja kiongozi wao huyo mahabusu.
Wakati wa kuwasili ndani ya chumba cha mahakama Zumaridi ameonekana akiwa amejifunika na kitenge wakati wote kisha akalazimika kukiondoa baada ya kupanda kizimbani kusomewa maelezo hayo
Akiahirisha kesi hiyo leo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Stella Kiama alisema shauri hilo litatajwa tena hapo Aprili 18 mwaka huu, baada ya kutokuwepo kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, aliyeanza kusikiliza kesi hiyo tangu awali, Monica Ndyekobora kutokana na kuwa safarini.
Watuhumiwa wanane ambao ni wafuasi wa Zumaridi wamepata dhamana baada ya kukataa kupatiwa dhamana siku ya kwanza kesi hiyo ilipotajwa, kwa madai ya kukaa na mhubiri wao pamoja hadi atoke.
Kwa sasa watuhumiwa waliobaki ni wanane ikiwa ni mabadiliko, baada ya kubadili misimamo yao ya awali waliyojiwekea ya kuendelea kukaa na mhubiri huyo.
Wakili wa upande wa walalamikiwa Erick Muta, alisema wafuasi wengine saba wanakamilisha taratibu za kuomba kupata dhamana, ili waweze kutoka mahabusu.
Mhubiri huyo wa Kanisa la Zumaridi, alikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo Februari mwaka huu kwa makosa ya usafirishaji na utumikishaji wa watu kwa kisingizio cha imani ya dini, ambapo ilipotajwa kwa mara ya kwanza ilielezwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wakusikiliza shauri hilo na kuahirishwa.
Awali Mawakili wa Serikali Waandamizi, Emmanuel Luvinga na Gisela Bantulaki, waliiomba mahakama hiyo kutoendekeza baadhi ya watuhumiwa kutofika mahakamani hapo, kwa visingizio vyovyote vile, baada ya mshitakiwa mmoja kushindwa kufika mahakamani kwa madai ya kuwa na majukumu ya kikazi.
Zumaridi katika kesi namba 11 ya mwaka 2022, anatuhumiwa kusafirisha watu na kumpiga Ofisa wa Polisi kwa kushirikiana na wenzake walipokuwa wameenda kwenye eneo lake, baada ya kuwepo malalamiko dhidi yake.
Pia upande wa Jamhuri uliomba kesi zote, ikiwa ni pamoja na kesi namba 10 na 12 za mwaka 2022 zinazowakabili na wenzake zaidi ya 90 ziahirishwe kutokana na kutokuwepo Hakimu Monica Ndyekobora.