Wagonjwa 161, wathibitishwa kuwa na UVIKO-19 nchini Tanzania.

Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema idadi ya maambukizi mapya ya Ugonjwa wa Virusi vya Uviko-19 imeongezeka na kufikia 161 ikilinganishwa na maambukizi 68 kwa kipindi cha Aprili 2 hadi Mei 4, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali nchini humo, Dk Aifello Sichwale imeeleza kuwa ongezeko hilo ni sawa na asilimia 137, hali inayoashiria kuwa maambukizi yameanza kuongezeka kwa jamii.

Taarifa hiyo imeeleza katika kipindi cha miezi miwili mfululizo hakuna kifo kilichoripotiwa.

Mchanganuo wa idadi ya waliothibitika katika kipindi cha Mei 5 hadi Juni 3, 2022 inaonesha kuwa Dar es Salaam uliripoti visa 130, Arusha (10), Mwanza (5), Shinyanga (4), Mtwara (3), Dodoma (2), Mara (2), Morogoro (1), Simiyu (1), Katavi (1), Kilimanjaro (1) na Mbeya (1), jumla ya wagonjwa watatu (3) waliothibitika kuwa na Covid-19 walilazwa na wote walikuwa hawajapata chanjo.

“Kwa takwimu hizi, inaonyesha kuwa, chanjo ni kinga dhidi ya madhara ya uviko-19, Serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo nchini ili kuwezesha wananchi kupata kinga dhidi ya ugonjwa huu” imesema sehemu ya taarifa hiyo

Aidha kwa mujibu wa Mganga Mkuu, kuanzia Mei 5 hadi Mei 3 Juni 2022 jumla ya wananchi waliopata dozi kamili ya chanjo ya uviko-19 19 ni 775,680, hivyo Wizara inaendelea kuwasisitiza wananchi kupata na kukamilisha dozi za chanjo ili kuzuia kupata maambukizi ya UVIKO-19.