Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imetupilia mbali ombi la dhamana ya Wakili maarufu nchini Tanzania, Peter Madeleka lililoombwa mahakamani hapo jana na jopo la mawakili watano wanaomtetea.
Uamuzi huo mdogo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 40/2020 umetolewa leo Jumanne Agosti 1, 2023 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa ambaye amesema kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Julai 17, 2023 ambao uliondoa makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining), hivyo hata hati ya mashitaka iliyofanyiwa marekebisho ambayo ilikuwa na makosa yenye dhamana nayo imefutwa.
Amesema kilichoamuliwa na Jaji Aisha Bade wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ni kuondoa makubaliano hayo ambayo yalifanyika Aprili 27, 2021.
Amesema baada ya kufutwa mwenendo huo hati inayomshitaki ni ya awali ambayo ina makosa 10 ikiwemo utakatishaji fedha lisilo na dhamana kisheria hivyo mshitakiwa ataendelea kukaa mahabusu.
Madeleka anatetewa na jopo la mawakili watano wakiongozwa na Wakili Boniface Mwabukusi, huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wa Serikali watatu wakiongozwa na Upendo Shemkole.
Baada ya uamuzi huo mdogo Hakimu Mbelwa aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15, mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Wakili Mwabukusi amesema wanatarajia kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo mdogo wa mahakama hiyo ya chini.
“Tunaamini kisheria hati ikishabadilishwa ile ya awali inakuwa haipo, hivyo tutazungumza na mteja wetu na tutakwenda Mahakama Kuu kudai haki yake ya dhamana.
“Tunaamini hati ya mashitaka ni suala la kisheria na kuna msimamo wa kisheria pale unapokuwa umefanya marekebisho ya hati ile hati ya awali inakuwa hapo na tunaamini hati iliyofanyiwa marekebisho ambayo haina kosa la utakatishaji fedha ndiyo hati halali na si vinginevyo,” amesema.
Jana Julai 31, 2023 mawakili hao waliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja wao baada ya Wakili Upendo kueleza mahakama upelelezi haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine ya kutaja shauri hilo, ambapo Madeleka anashikiliwa katika mahabusu ya Gereza la Kisongo Arusha tangu Julai 17, 2023 alipokamatwa.
Kwa upande wake Wakili Mwabukusi aliwasilisha ombi la dhamana akisema, kwa kuwa shtaka linalomkabili mteja wao lina dhamana na kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika, mahakama impe mteja wao haki yake ya dhamana kwa masharti nafuu yatakayomwezesha kufikia haki hiyo.
Hata hivyo, Wakili Upendo aliwasilisha ombi kwa Mahakama hiyo akitaka imnyime dhamana washtakiwa akidai katika kesi inayomkabili ana makosa10 ikiwemo utakatishaji fedha ambalo halina dhamana.