Wakili wa kujitegemea nchini Tanzania Peter Madeleka amekamatwa na Jeshi la polisi katika Kituo Jumuishi cha utoaji haki nchini humo baada ya kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Madeleka kabla ya kukamatwa alilazimika kung’ang’ania kwa zaidi ya Dakika 30 katika chumba cha Mahakama (chember court) cha Jaji Aisha Bade ambaye awali ndiye alitoa maamuzi katika kesi yake ya kupinga makubaliano ya kukiri kosa.
Baada ya kufika Wakili wake, Simon Mbwambo na wanahabari ndipo, Wakili Madeleka alitoka ndani ya chumba cha Mahakama na baadae kuchukuliwa na polisi.
Awali Wakili Madeleka alisema alikuwa amefungua kesi katika Mahakama Kuu, kupinga maamuzi ya Hakimu Mkazi Arusha, kumtia hatiani katika kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Amesema baada ya hukumu hiyo, alilazimishwa kufanya makubaliano ya kukiri kosa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na baada ya kuachiwa alikata rufaa.
“Katika maamuzi ya leo ambayo awali yalipangwa kufanyika Ijumaa wiki iliyopita, Jaji Bade amekubaliana na hoja yangu kuwa upande wa mashtaka kabla ya kuingia katika makubaliano ya kukiri makosa ulipaswa kuwa na ushahidi wa kosa nililotenda,” amesema.
Hata hivyo, Jaji Bade ameagiza kesi hiyo kuanza upya kusikilizwa katokana na baadhi ya mapungufu katika shauri hilo.
Wakili wa Madeleka, Simon Mbwambo hata hivyo amesema hajui kosa ambalo mteja wake anakabiliwa nalo kwa sasa.
“Sijui kosa naona polisi wamemkata na wanampeleka Ofisi ya RCO (Mkuu wa Upelelezi Mkoa Arusha) kwa mahojiano, labda wanataka kuanza upya kusikiliza kesi hii ya leo,” amesema.
Polisi waliomkamata Wakili Madeleka hata hivyo hawakuwa tayari kuelezea tuhuma zake na kuwataka wanahabari kufuata taratibu za kupata habari kwa kuzungumza na viongozi wa juu wa polisi.
Wakili Madeleka katika siku za karibuni amekuwa katika harakati za kupinga Mkataba wa Bandari na wiki iliyopita alikuwa jijini Dar es Salaam katika mkutano ulioandaliwa na Balozi mstaafu Dk Wilibroad Slaa na Wakili Boniface Mwabukusi.