Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), leo wanakutana katika Mkutano Maalumu wa 19 unaofanyika jijini Arusha kujadili Ripoti ya Baraza la Mawaziri kuhusu suala la uanachama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya EAC, Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano Maalumu wa 48 wa Baraza la Mawaziri wa EAC, uliofanyika Ijumaa Machi 25, 2022 kujadili ajenda na programu ya Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi za EAC.
Mkutano huo utaoneshwa moja kwa moja kwenye tovuti ya EAC – www.eac.int pamoja na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii ya EAC.
Kuingia kwa DRC katika EAC kutaifanya jumuiya hiyo ya kikanda kuwa na nchi saba wanachama za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na DRC itakayokuwa mwanachama wa saba ikifuatia Sudan Kusini iliyojiunga mwaka 2016.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, kujiunga kwa DRC katika EAC kutakuwa na tija kibiashara kwa mataifa yote wanachama. Chanzo kimoja kinasema: “Utulivu na usalama katika ukanda huo mzima utafanikisha juhudi za kuboresha hali za kimaisha za wakazi wake, kutokana na utajiri wa kilimo, maliasili na nguvu kazi ya nchi zote kwa pamoja.”
Kinaongeza: “DRC isiyo na bandari, upande wa Mashariki, kupitia bandari kuu za Mombasa na Dar es Salaam kutakuwa na fursa adhimu ya kuongeza usafirishaji wa bidhaa zake huku ikinufaika kwa kuondolewa masharti ya awali ilipokuwa nje ya jumuiya.”