Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa idhini kwa wanafunzi 337 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022 na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kurudia mtihani huo.
Wanafunzi hao walifutiwa matokeo kwa sababu mbalimbali ikiwemo udanyanyifu na wakaomba kupewa nafasi ya kurudia mtihani huo.
Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa ruhusa hiyo ni kwa wanafunzi wote waliofutiwa matokeo wakiwemo wanafunzi wanne waliofutiwa kwa kuandika matusi.
“Tungesema hawa wanafunzi warudie mitihani na wenzao wa kidato cha nne kwa utaratibu wa kawaida kama ilivyozoeleka serikali ingepata hasara zaidi ya Sh bilioni moja ila kwa utaratibu huu wa kuomba wenyewe kama na kufanya mtihani huo pamoja na wenzao wanaofanya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu kwa utaratibu utakaowekwa na NECTA basi itasaidia sana kupunguza gharama,” amesema Prof. Mkenda.
Utaratibu wa kurudia mitihani kwa wanafunzi hao utakwenda sambamba na mitihani ya kidato cha sita ambao unatarajiwa kuanza Mei 2, 2023, hivyo watawekewa utaratibu wa kuchanganyika pamoja wakati wa kurudia mitihani hiyo.
Pia amewataka watanzania kukemea kwa pamoja matukio ya wizi wa mitihani kwani inafundisha watoto udanganyifu na kuondoa weledi na kuwanyima haki watahiniwa ambao hawajashiriki katika wizi huo.