Jeshi la Polisi jijini Mwanza linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Nicholus Telesphory (25) na dereva taksi, Respikius Anastaz (55).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi amesema watu hao walikamatwa maeneo tofauti mkoani humo.
Ng’anzi amesema Januari 29, 2022 katika mtaa wa Ng’washi kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana mwanafunzi wa SAUT aliyekuwa akisoma shahada ya kwanza ya Uhusiano wa Umma na Masoko, Nicolaus Telesphory aliuawa kwa kushambuliwa na kundi la watu wakimtuhumu kuiba televisheni.
Amesema kwa sasa wanaoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi huyo ni watu watano
“Marehemu alifariki akiwa katika hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa kutumia mawe na fimbo kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake,” amesema Ng’anzi
Katika tukio lingine Kamanda Ng’anzi amesema Jeshi hilo linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za mauaji ya dereva taksi, Respikius Anastaz (55), baada ya kumnyonga kwa kamba shingoni kisha kumchoma na kisu katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Kwa mujibu wa Kamanda Ng’anzi, tukio hilo lilitokea Januari 26 mwaka huu usiku katika kijiji cha Kasungamile wilayani Sengerema mkoani humo.
Kamanda huyo amebainisha kwamba baada ya watuhumiwa hao kufanya mauaji walikimbilia nyumbani kwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya kufanyiwa zindiko ili wasibainike kuhusika kwenye mauaji hayo.
“Baada ya kutekeleza mauaji hayo watuhumiwa walitelekeza gari la dereva na kukimbilia kwa mganga wa kienyeji ndipo gari ya polisi iliyokuwa kwenye doria ilipotilia mashaka kari hiyo na kwenda kukagua na kukuta mwili wa dereva huyo ukiwa umetobolewa katika maeneo mbalimbali,”
Ameongeza kuwa “Baada ya kukuta mwili wa dereva huyo ndani ya gari maofisa wa jeshi letu walifanya upelelezi hadi jijini Mwanza na kugundua gari hiyo ilivuka na kina nani, nani alikatisha tiketi na watu waliokuwa na marehemu, usiku huo huo askari waligundua kuwa watuhumiwa wameenda kwa mganga wa jadi wakizindikwa ili wasikamatwe na polisi,” ameongeza Ng’anzi
Pia Ng’anzi amesema kupitia upelelezi huo walifanikiwa kumkamata mganga wa jadi na mkewe kwa tuhuma za kuhusika katika tukio hilo.
Ametoa wito kwa jamii na watu wenye nia ya kufanya uhalifu kuacha kufanya hivyo huku akionya kwamba Jeshi hilo halitosita kumchukulia hatua kali yoyote atakayebainika kufanya hivyo.