Wafanyabiashara ndogondogo nchini Tanzania maarufu kama machinga wa soko la Karume wameandamana hadi kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla wakimshinikiza kiongozi huyo kutoa tamko la kuwaruhusu waendelee kufanya shughuli zao kwenye soko hilo, ambalo liliteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabishara hao wamesema wanafanya hivyo kwa sababu wamekosa imani kuhusu maamuzi yaliyochukuliwa na viongozi wa Serikali, na wanashangazwa na vitendo vya jeshi la Polisi kuvunja mabanda yao waliyoyajenga usiku wa kuamkia leo.
“Tumekosa imani na viongozi jana alisema anakuja lakini hadi sasa hatujamuona na cha kushangaza waliojenga vibanda vyao wamebomolewa, sisi hatuwezi kuwasubiri wao maisha yetu magumu watuache tujenge wenyewe ili tuendelee kufanya kazi zetu“
Wamesema siku zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kufanya uchunguzi ni nyingi hivyo wameiomba Serikali iwaachie hivi sasa waweke biashara zao ili wafanye biashara zao wakati ambapo uchunguzi unaendelea kufanyika ili waweze kupata pesa za chakula na za kurudisha mikopo waliyonayo.
Itakumbukwa kuwa jana baada ya soko hilo kuungua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla aliwataka wafanyabiashara wa soko hilo kuwa watulivu na kuahidi kuwa itaundwa kamati ambayo itachunguza chanzo cha moto huo kwa siku 14 huku akipiga marufuku shughuli zozote kuendelea wakati wa uchunguzi huo.
Hata hivyo muda mfupi baada ya RC Makalla kutoa tamko hilo, Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa aliagiza kamati hiyo kufanya uchunguzi kwa siku saba na si siku 14.
Hii leo Mkuu wa wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija amewaomba wafanyabishara hao kuwa wavumilivu na kufuata utaratibu uliotangazwa na Serikali kwamba waiachie kamati ifanye kazi kwa siku saba na kutoa ripoti badala ya kuandamana kutaka kushindana na Serikali.
“Mnatakiwa kujiongeza pamoja na kwamba mnadai haki lakini lazima mfuate utaratibu Jana Waziri tuiachie Kamati ifanye kazi na walete ripoti tunaomba kuweni na subira” amesema.
Hata hivyo kauli ya mkuu huyo wa wilaya haiukufua dafu bali ilionekana kuongeza gadhabu kwa wafanya biashara hao ambao mbali na kuandamana katika ofisi hiyo wamefunga barabara huku wakiimba nyimbo yenye maneno machache kuwa “Tunataka Soko letu”
Hivi karibuni kumekuwa na historia mbaya ya masoko kuungua moto na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara huku vyanzo vya moto visijulikane licha ya tume za uchunguzi kuundwa.
Miongoni mwa masoko yaliungua ni pamoja na soko kuu la Kariakoo, soko la Makoroboi lililopo jijini Mwanza, soko la Tunduma, soko la uhindini lililopo jijini Mbeya pamoja na soko la Karume ambalo limeungua usiku wa kuamkia jana.