Wanaharakati wa mitandaoni, Innocent Paul Chuwa maarufu kama Kiduku, na Farida Mikoroti, waliokamatwa kwa tuhuma za makosa ya mtandao, wameachiwa kwa dhamana kutoka Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati (Central Police) Dar es Salaam, Jumatano Oktoba 01, 2025.
Wawili hao wameshikiliwa kwa takribani juma moja tangu kukamatwa kwao, huku wakielezwa kuwa licha ya dhamana hiyo, watalazimika kuripoti kituoni kila siku asubuhi. Polisi pia wamesema kuwa muda wowote wanaweza kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mawakili waliokuwa mstari wa mbele kufuatilia dhamana hiyo ni Kulwa William Maduhu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Paul Kisabo kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), na Fredrick Msaki kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Wote walishirikiana kuhakikisha kuwa wanaharakati hao wanapewa haki zao kisheria katika mchakato mzima wa dhamana.