Wanajeshi wawili wa Tanzania wauawa katika mapigano DRC

Wanajeshi wawili wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameuawa katika mapigano yaliyotokea katika kipindi cha siku kumi zilizopita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Shambulizi kutoka kwa kundi la waasi la M23, ambalo linapata msaada kutoka Rwanda, ambalo limechukua mji mkuu wa Goma na kuahidi kuendelea hadi mji mkuu wa Kinshasa, limewakasirisha wachambuzi wa kimataifa.

Hii ni hatua nyingine ya kuongezeka kwa mapigano katika eneo lenye rasilimali nyingi za madini ambalo limekuwa na vita kwa miongo kadhaa likihusisha makundi ya waasi kadhaa.

Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walitumwa chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kufanya kazi mashariki mwa DR Congo.

“Kufuatia mashambulizi kadhaa yaliyofanyika katika maeneo ya Sake na Goma yaliyofanywa na waasi wa M23 tarehe 24 na 28 Januari 2025, JWTZ imepoteza wanajeshi wawili,” amesema Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda 

Alithibitisha kuwa wanajeshi wanne wengine walijeruhiwa na sasa wanapatiwa matibabu Goma.

Ilonda alisema vitengo vilivyobaki  bila kutoa maelezo zaidi  “vinaendelea kutekeleza majukumu yao chini ya mwongozo wa SADC.”

Aliongeza kuwa maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kurejesha miili ya wanajeshi wa Tanzania.

Hadi sasa, wanajeshi 13 wa Afrika Kusini, watatu wa Malawi, na raia mmoja wa Uruguay wameuawa katika mapigano hayo ya DR Congo.

Mapema wiki hii, SADC iliita mkutano wa pamoja na Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) kuhusu mgogoro huu.

Jumapili, Rwanda ilisema itakaribisha mkutano huo, huku pia ikikosoa ushiriki wa SADC katika mgogoro wa DR Congo.

Rwanda haijawahi kukiri kujihusisha kijeshi na msaada kwa kundi la M23, hata hivyo, ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Julai mwaka jana ilisema Rwanda ina takribani wanajeshi 4,000 mashariki mwa DR Congo, na ilikosoa Kigali kwa kudaiwa kuwa na “udhibiti halisi” juu ya kundi hilo.

Rwanda inadai kuwa DR Congo inasaidia na hifadhi kundi la FDLR, kundi la waasi lililoanzishwa na viongozi wa zamani wa Hutu walioua Watusi katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.