Wanawake waongoza kwa kuugua ugonjwa wa saratani

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) imesema kati ya wagonjwa wapya 8,000 na wale wa marudio 68,000 waliopokelewa mwaka 2021 asilimia 70 ni wanawake.

Licha ya saratani ya kizazi na ile ya matiti zinazowahusu wanawake kuongoza, imeelezwa kuwa wanawake pia wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa katika saratani zingine zikiwemo saratani za utumbo mpana, njia ya chakula, ngozi na hata saratani ya damu.

Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage amesema idadi ya wagonjwa wa Saratani inaongezeka kila mwaka 

“Kwa mwaka tunaona wagonjwa wapya 8,000 na wale wagonjwa wanaorudia ni 68,000 lakini katika hawa wote, asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani ni wanawake na asilimia 30 ni wanaume,” amesema Dk Mwaiselage.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekiri kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake wanaougua Saratani.

“Asilimia 70 ya wagonjwa ni wanawake lakini pia tukumbuke kuwa wanaouguza wagonjwa wa saratani pia ni wanawake, hili ni suala pana la kuangalia na tushushe huduma za uchunguzi katika ngazi za chini ili kuwaokoa wengi katika hatua za awali,” amesema.

Waziri Ummy ametaja pia kuongezeka kwa saratani ya tezi dume kutoka asilimia 1 mpaka kufikia asilimia 6.

“Mwaka 2018 kulikuwa na wagonjwa wapya 150 hapa Ocean Road lakini kwa mwaka 2021 wameongezeka mpaka kufikia 531. Ni lazima tuchunguze katika hili inaweza kuwa sababu tumeongeza huduma za uchunguzi na kipimo rafiki kwa wanaume, lakini tuendelee kuwahamasisha tezi dume inatibika ikigundulika mapema,” amesema.