Wasiojulikana wamuua mwanamke wa miaka 27, nchini Tanzania

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao

Mwanamke mmoja nchini Tanzania  aliyefahamika kwa jina la Leah Emmanuel (27), mkazi wa Mtaa wa Mtakuja Manispaa ya Tabora ameuawa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na kushambuliwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema mauaji hayo yametokea Machi 22,2022 majira ya saa nane mchana katika mtaa huo na watu ambao bado hawajajulikana.

“Mkazi huyo ameshambuliwa kwa kukatwa katwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake, chanzo cha mauaji haya bado haijajulikana kwani bado tunaendelea na uchunguzi” amesema. Kamanda Abwao

Aidha metoa wito kwa wakazi wa Tabora kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwabaini wahusika waliofanya tukio hilo.

Bado wimbi la visa vya mauaji nchini Tanzania linaendelea, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa matukio hayo mengi yanasababishwa na wivu wa mapenzi, mali na imani za kishirikina