Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Stephen Wasira amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo hakina hoja ya msingi ya kuzuia Uchaguzi Mkuu mwaka huu kwani kama ni mabadiliko wanayoyazungumza yameshafika tayari.
Amesema CHADEMA wao wanasema hawataki uchaguzi mpaka yafanyike mabadiliko ya uchaguzi, lakini ukweli wameshafanya marekebisho, na kusisitiza marekebisho yaliyofanyika yanahusisha sheria tatu ambazo zimefanyiwa mabadiliko.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana Machi 27,2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kahama,Wasira aliyekuwa akihutubia wananchi hao amesema sheria zilizofanyiwa mabadiliko ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na madiwani.
Amesema nyingine ni sheria nyingine ni ya Tume ya uchaguzi pamoja na sheria ya vyama vya siasa vinavyosimamiwa na msajili wa vyama vya siasa na kuongeza mambo hayo ndiyo waliyokuwa wanalalamikia.
“Moja wanasema wao hawataki uchaguzi wanasema tume ile inateuliwa na Rais moja kwa moja kwahiyo sio huru, tukasema hamna tabu sheria mpya wabunge wako hapa, wakaunda kwamba tuweke kamati maalumu ili mtu anayetaka ukamishna wa tume ya uchaguzi waombe na ipo hiyo inaongozwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar na watu kutoka Tume ya Haki za Binafamu na Utawala Bora.
“Kwahiyo ukifika wakati atakayetaka ukamishna anaomba na huyo anayeomba anatazamwa kwa vigezo vilivyowekwa kulingana na kazi anayoomba ,hiyo kamati ipo na maana yake ni kwamba mamlaka ya Rais yamepunguzwa…zamani alikuwa anaweza kuteua sasa hawezi, mpaka kamati ya usaili halafu imuambie Rais umehitaji watu watano tunakupa wanane chagua watano.”
Wasira amesema hayo ni mabadiliko makubwa na kuongeza wapinzani walisema Wakurugenzi watendaji wa halmashauri wanaiba kura hivyo hawataki wasimamie uchaguzi na walienda mpaka Mahakama ya Afrika Mashariki kupinga wakurugenzi hao ,hivyo sheria mpya imewaondoa.