Wakati Watanzania wakijiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kesho Jumatano, shughuli mbalimbali zimeendelea leo Jumanne katika pande zote mbili za Muungano, zikihusisha kufungwa kwa pazia la kampeni Tanzania Bara na kuanza kwa kura ya mapema visiwani Zanzibar.
Wapiga kura visiwani Zanzibar leo wameanza kushiriki katika zoezi la kupiga kura ya mapema, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika kesho, Oktoba 29. Kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya Uchaguzi ya mwaka 2018, Zanzibar imepewa mamlaka ya kuendesha kura ya mapema kabla ya siku rasmi ya uchaguzi. Kwa uchaguzi huu wa mwaka 2025, kura hiyo inafanyika leo Jumanne, Oktoba 28.
Uchaguzi huo unamkutanisha Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayewania muhula wa pili, na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, wa chama cha ACT-Wazalendo. Hata hivyo, chama hicho cha upinzani kimepinga utaratibu wa kura ya mapema, kikidai kuwepo kwa dosari katika mchakato huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa 1:00 asubuhi na vitafungwa saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, huku matokeo ya uchaguzi wa urais visiwani humo yakitarajiwa kutangazwa ndani ya saa 72 baada ya vituo kufungwa. Kampeni za uchaguzi huo zilianza Septemba 11 na kukamilika Jana, Oktoba 27.
Wakati huo huo, Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa leo kuhitimisha rasmi kampeni zake kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Viwanja vya CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Samia, mwenye umri wa miaka 65, anaingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa kesho akiwa na historia ya kipekee kama mwanamke wa kwanza kuidhinishwa na CCM kugombea nafasi ya urais wa Muungano. Kabla ya hapo, aliweka historia nyingine kwa kuwa Makamu wa Rais na baadaye Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, katika kipindi cha siku 60 za kampeni, Samia amefanya mikutano ya hadhara 114 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kupitia Ilani ya Uchaguzi ya 2025–2030, ameahidi kuendeleza mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kujenga uchumi wa kisasa, jumuishi na shindani; kuongeza ajira kwa vijana; kupunguza umaskini; na kuboresha ustawi wa wananchi. Pia ameahidi kudumisha demokrasia na utawala bora kwa kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya.
Tangu aingie madarakani mwaka 2021, Dkt. Samia amekuwa akisistiza falsafa yake ya “4R” — Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding — inayolenga kujenga maridhiano na mshikamano wa kitaifa. Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wameeleza kuwa falsafa hiyo imekumbwa na changamoto kutokana na tuhuma za ukandamizaji wa kisiasa na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Leo pia ni siku ya mwisho ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo vyama 18 vya siasa vimekuwa vikihitimisha mikutano yao katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama 17 kati ya hivyo vina wagombea wa urais, baada ya chama cha ACT-Wazalendo kuondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa upande wa Tanzania Bara.
Tume hiyo, inayosimamia uchaguzi huu wa saba tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, imesema maandalizi yote yamekamilika kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024.
Baadhi ya vyama kama ADA-TADEA, NCCR-Mageuzi na NRA vilihitimisha kampeni zao mapema wiki hii, huku vyama vikubwa vikiendelea na mikutano mikubwa ya kufunga pazia leo katika majiji na mikoa mbalimbali. Watanzania wanatarajiwa kuenda vituoni kesho Jumatano, Oktoba 29, kupiga kura katika uchaguzi utakaowachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge, wawakilishi na madiwani.
Tume zote mbili INEC kwa Tanzania Bara na ZEC kwa Zanzibar zimeahidi kufanya uchaguzi ulio huru, wa amani na unaozingatia sheria. Mashirika ya kiraia na waangalizi wa kimataifa pia wanatarajiwa kufuatilia mchakato huo unaotazamwa kama kipimo muhimu cha demokrasia nchini.
Lakini ikumbukwe kuwa uchaguzi huu unafanyika ikiwa chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) hakishiriki uchaguzi huo baada ya kutangaza hapo awali kutoshiriki kwa madai kuwa mifumo ya uchaguzi imekuwa kandamizi.
Mwenyekiti wake ambaye Tundu Lissu, kwa sasa yupo gerezani kwa mashtaka ya Uhaini.