Watoto 10 walawitiwa na kubakwa katika kipindi cha miezi mitatu mkoani Shinyanga.

Watoto 10 wakazi wa Kata ya Mhongolo, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wamebakwa na kulawitiwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita na wengine wawili wakiliwa na fisi.

Waliofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka sita hadi 12 wa jinsia ya kike na walikutwa na mkasa huo baada ya kuagizwa na wazazi wao dukani nyakati za usiku.

Watoto wawili wa kike walioliwa na fisi wanatoka katika kata za Ngogwa na Wendele huku sababu ikitajwa kuwa ni kutokana na kuwapo mashamba makubwa ambayo wanyama hao wanajificha.

Akitoa taarifa ya matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2022, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Tiho Masatu, amesema wazazi na walezi wamekuwa wakichangia kusababisha watoto wao wa kike kufanyiwa vitendo vya kikatili hususani kubakwa na kulawitiwa na watu wasiojulikana kwa kuwaagiza nyakati za usiku kwenda dukani kufuata mahitaji ya nyumbani.

“Vitendo vya ubakaji na ulawiti vimekithiri sana katika kata ya Mhongolo eneo la mtaa wa Mbulu na sababu kubwa inaonyesha ni vitendo vya wazazi kuwa na tabia ya kuwatuma watoto madukani hususani nyakati za usiku,” alisema Masatu.

Masatu amewataka wazazi kuhakikisha wanakuwa makini katika kulinda watoto wao hususani wa jinsia ya kike ili kuepukana na vitendo hivyo kwa kuwa vimekuwa vikiwaathiri na kushindwa kuendelea na masomo yao shuleni.

Kuhusu watoto kuliwa na fisi, Masatu alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na idara ya wanyamapori wameanzisha msako wa kuwatafuta wanyama hao ili kuwatokomeza.

Hata hivyo, alisema mpaka sasa hakuna hata mnyama mmoja aliyekamatwa na kuuliwa na kwamba wamekuwa wakifanya kazi hiyo mara kwa mara.

Masatu aliitaka jamii kuacha kuhusisha matukio hayo na imani za kishirikiana na kuwataka kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wanawatokomeza wanyama hao.