Arbay Mahad Qasim tayari amepoteza watoto wawili kutokana na ukame mbaya, na sasa mwanakijiji huyo wa Somalia anahofia kuwa anaweza kupoteza mtoto wa tatu huku mtoto wake mdogo Ifrah akisubiri matibabu katika hospitali ya Mogadishu.
Qasim ni miongoni mwa wazazi wengi waliojazana katika Hospitali ya Banadir and Maternity Hospital ambayo imeshuhudia wagonjwa wengi wanaofika katika hospitali kutokana na janga la njaa linaloikumba Somalia kote huku ukame ukiikumba Pembe ya Afrika.
Vijiji vingi vimelazimika kuyahama makazi yao baada ya mvua kunyesha na kuharibu mazao na kuua mifugo.
Mvua ilipokosa kunyesha kwa msimu wa nne mfululizo mwezi uliopita, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na wataalamu wa hali ya hewa walionya kuwa njaa huenda ikakumba nchi za Somalia, Kenya na Ethiopia.
Lakini kwa Wasomali wengi kama Qasim, ambaye amekuwa akiishi kwa msaada wa serikali kwa miezi michache iliyopita, janga tayari limemfika.
Watoto wake wawili walikufa kwa njaa katika miezi 18 iliyopita.
Hali ya Afya ya Ifrah mwenye umri wa miaka miwili ilipoanza kudhoofika, alionyesha dalili za utapiamlo mkali, Qasim hakupoteza muda, alitumia siku moja kusafiri hadi Mogadishu kutoka kijijini kwake kusini-magharibi katika jitihada za kuokoa maisha ya mtoto wake mdogo.
Wengine wametembea kwa siku nyingi kutafuta msaada, wakiwa wamebeba watoto wao wachanga wagonjwa migongoni mwao.
Wengi wameliambia shirika la habari la AFP kuwa hawajawahi kustahimili janga la kutisha kama hili wanaloshuhudia kwa sasa, wakirejelea maonyo ya wanasayansi wa hali ya hewa ambao wamesema ukame wa sasa ndio mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo minne.
“Mazao hayakufaulu. Tulipoteza mifugo. Mto ulikauka,” Khadija Mohamed Hassan, ambaye mtoto wake Bilal mwenye umri wa miezi 14 ni miongoni mwa waliolazwa katika kituo cha Banadir.
“Nina umri wa miaka 45 na sijawahi kuona ukame mbaya kama huu maishani mwangu. Tunaishi katika hali mbaya sana.”
Wahudumu wa afya tayari wamezidiwa, huku daktari Hafsa Mohamed Hassan akiiambia AFP kwamba idadi ya wagonjwa wanaofika katika kituo cha Banadir kutokana na utapiamlo imeongezeka mara tatu tangu ukame uanze na hivyo kusababisha uhaba wa vitanda kwa wagonjwa wengine.
“Kesi tunazopokea ni pamoja na watoto wenye matatizo mengine ya kiafya kama surua kali na wengine ambao wako katika hali ya kukosa fahamu kutokana na utapiamlo mkali,” alisema.
Hali inaelekea kuwa mbaya zaidi, alisema Bishar Osman Hussein wa shirika lisilo la kiserikali la Concern Worldwide, ambalo limekuwa likisaidia kituo cha Banadir tangu 2017.
“Kati ya Januari na Juni mwaka huu, idadi ya watoto waliolazwa katika kituo cha Hospitali ya Banadir wakiugua utapiamlo mkali na matatizo mengine imeongezeka kutoka 120 hadi 230 kwa mwezi,” aliiambia AFP.
Wataalamu wa hali ya hewa wameonya kuwa mvua ya masika ya Oktoba-Novemba inaweza pia kutonyesha na hivyo kutumbukiza eneo hilo katika janga zaidi.
Somalia imekumbwa na migogoro na haina vifaa vya kutosha vya kukabiliana na mzozo huo, huku kukiwa na waasi wa Kiislamu wanaozuia ufikiaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo ya nchi.
Maelfu ya maili mbali, vita vya Ukraine pia vimekuwa na athari mbaya kwa maisha ya Wasomali, huku bei ya vyakula ikipanda na usaidizi ukiwa haba.
Baadhi ya Wasomali milioni 7.1 — karibu nusu ya wakazi — wanapambana na njaa, huku zaidi ya 200,000 wakikabiliwa na baa la njaa, Umoja wa Mataifa ulisema wiki hii.
Wakati huo huo maombi ya msaada kwa kiasi kikubwa hayajazingatiwa, huku mashirika yakikusanya chini ya asilimia 20 ya fedha zinazohitajika kuzuia kutokea kwa njaa ya mwaka 2011 ambayo iliua watu 260,000 — nusu yao wakiwa watoto chini ya umri wa miaka sita.
“Hatuwezi kusubiri njaa kutangazwa kama hali ya dharura kabla kuchukua hatua,” El-Khidir Daloum, mkurugenzi wa nchi wa Mpango wa Chakula Duniani nchini Somalia, alisema katika taarifa yake Jumatatu.
Huku misaada ya kibinadamu ikipungua, Rais mteule wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amewataka Wasomali kuwasaidia raia wenzao.
“Mtu yeyote aliye na sahani ya chakula kwenye meza yake leo lazima afikirie kuhusu mtoto ambaye analia mahali fulani kwa sababu ya njaa na kuwasaidia kwa njia yoyote iwezekanavyo,” alisema wakati wa ziara ya hivi majuzi kwenye kambi ya makazi ya jamii zilizohamishwa na ukame.
Katika hospitali ya Banadir, Khadija Mohamed Hassan anakaa macho akimshughulkia Bilal ambaye mwili wake umesalia mifupa tu kutokana na utapiamlo mkali na uliojaa mirija na bandeji.
“Tumekuwa hapa kwa siku 13, na anaonekana kupata nafuu sasa” alisema.