Watu 14 wahofiwa kufa maji baada ya mitumbwi kuzama mkoani Mara

Watu 14 wanahofiwa kufa maji mkoani Mara baada ya mitumbwi miwili waliokuwa wamepanda kuzama, wakati wakitoka kanisani katika kisiwa cha Mchigondo kilichopo wilayani Bunda.

Tukio hilo limetokea jana Julai 30, 2023 majira ya jioni kufuatia hali ya upepo mkali.

Habari kutoka mkoani Mara zinaeleza kuwa mitumbwi hiyo miwili ilikuwa ikifuatana na ndipo upepo mkali ulipoanza na kusababisha mtumbwi mmoja kuzama na kusababisha mtumbwi mwingine kurudi nyuma Ili kuokoa na ndipo ilipozama yote.

Akizungumza na Mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mkoani Mara, mkuu wa mkoa huo Said Mtanda amekiri kupokea taarifa za tukio hilo ambapo amesema watu 13 wameokolewa wakiwa hai akiwemo mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja huku wengine 14 wakihofiwa kufa maji.

Mtanda amesema tayari mkuu wa wilaya ya Bunda, Dkt. Vicent Anney amefika eneo la tukio alfajiri ya leo kwa ajili ya kufuatilia tukio hilo.

Ameongeza kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na maafiisa wa Mamlaka nyingine pia wamekwishafika eneo la tukio na kwa sasa wanasubiri taarifa kamili.