Zaidi ya watu elfu nne wamefariki dunia katika ajali za barabarani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, huku wengine zaidi ya elfu tano wakijeruhiwa katika ajali hizo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa takwimu hizo huku akielezea kuwa hazifurahishi, kutokana na kuchukua uhai wa Watanzania licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kuboresha barabara hapa nchini.
Akifungua maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yanayofanyika Kitaifa mkoani Mwanza, Waziri Mkuu Majaliwa amesema elimu zaidi na udhibiti wa madereva inapaswa kuongezwa, ili kupunguza ajali zinazoendelea kuchukua uhai wa Watanzania.
Ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kutumia teknolojia za kisasa katika kudhibiti ajali za barabarani, ikiwa ni pamoja na kutambua madereva wanaovunja kwa makusudi sheria za babarani na kusababisha ajali.
Waziri Mkuu Majaliwa ametaka umakini kwa wamiliki wa mabasi yanayoenda masafa marefu, na kuhakikisha kunakuwa na madereva wawili katika kila basi linaloenda masafa marefu.